Kocha Mkuu wa timu ya vijana ya Tanzania umri chini ya miaka 17, Serengeti Boys Oscar Milambo ameomba radhi kufuatia timu hiyo kuondoshwa kwa aibu kwenye michuano ya AFCON U17 inayofanyika nchini kwa kufungwa michezo yote mitatu
Milambo amesema michuano hiyo itawasaidia kujitathmini na kufanya maandalizi mazuri zaidi kuweza kufanya vizuri michuano ijayo
"Kwa niaba ya benchi la ufundi, naomba kutumia nafasi hii kuwaomba msamaha watanzania ambao walikuwa na matarajio makubwa na vijana wao," amesema
"Sisi benchi la ufundi tulijua tumefanya maandalizi ya kutosha lakini bahati mbaya sana maandalizi yalikuwa hayatoshi kushinda haya mashindano"
"Mimi kama mkuu wa benchi la ufundi nawajibika moja kwa moja kwa kila ambacho kimetokea kwa sababu mpaka meli inazama mimi ndio nilikuwa nahodha"
"Tunaomba radhi kwa matokeo ambayo tumeyapata tunaamini kuna vitu vingi sisi kama benchi la ufundi tumejifunza lakini nchi imejifunza na kama kutakuwa na wakati mwingine wa kufanya maandalizi tunapaswa kufanya zaidi ya ambayo tumefanya ili kuweza kuyaishi matarajio yetu"