Kimahesabu Yanga bado ina nafasi ya kutwaa mataji mawili msimu huu kombe la FA na ligi kuu ingawa hili la pili litategemea zaidi na makosa ya wapinzani wao Simba ambao mpaka sasa hawaonekani kuyafanya
Taji la kombe la FA liko ndani ya uwezo wa Yanga kwani kama itashinda michezo miwili tu, mmoja wa nusu fainali dhidi ya Lipuli na mchezo wa fainali dhidi ya Azam Fc au KMC, itaweza kulitwaa
Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema wamedhamiria kupata tiketi ya kushiriki michuano ya CAF msimu ujao hivyo hawapaswi kufanya makosa katika michezo iliyobaki kwenye ligi na kombe la FA
Kwenye ligi Yanga imebaki na michezo 10 dhidi ya Ndanda Fc, Kagera Sugar, Ruvu Shooting, Tanzania Prisons, Azam Fc(2), Mtibwa Sugar, African Lyon, Biashara United na Mbeya City
Ili kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu, Yanga inapaswa kujiwekea malengo ya kushinda michezo yote 10 iliyobaki kwani sare au kupoteza mchezo kutainufaisha zaidi Simba ambayo imekuwa ikicheza michezo yake ikiwa viporo
Yanga itaanza kampeni ya ushindi katika michezo hiyo 10 keshokutwa Alhamisi, April 04 ambapo itakuwa mkoani Mtwara kupepetana na Ndanda Fc katika mchezo wa ligi kuu utakaopigwa uwanja wa Nangwanda Sijaona