Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu imekosa msisimko kutokana na kukosekana kwa ushindani uliosawa baina ya timu zinazoshiriki
Wakati timu nyingine zikiwa zimebaki na michezo saba kumaliza ligi, baadhi ya timu zina michezo zaidi huku Simba ikivunja rekodi kwa kuwa na michezo 16
Cha kushangaza zaidi kuna timu bado hazijacheza kabisa michezo ya mzunguuko wa kwanza mfano Yanga na Azam Fc, Simba na Coastal Union
Ni vema TFF kupitia bodi ya ligi kuu ikajitafakari na kufanyia kazi mapungufu makubwa yaliyojitokeza msimu huu ili kuhakikisha ligi inakuwa na hadhi, inatoa ushindani ulio sawa miongoni mwa timu zinazoshiriki
Kwa hali ilivyo sasa ni rahisi kabisa 'kubet' ni timu gani itatwaa ubingwa, na hili linatokana na mazingira yaliyotengenezwa
Timu moja inapokuwa na michezo mingi ya viporo inakuwa na faida ya kufahamu aina ya matokeo ambayo inapaswa iyapate
Misimu michache iliyopita klabu ya Simba iliwahi kugomea kucheza michezo yake hadi pale baadhi ya timu zilizokuwa na viporo zimalize, sababu walifahamu athari ya timu moja kuwa na faida ya kufahamu matokeo ya washindani wake kwani inakuwa rahisi kwao kujipanga kupata matokeo yatakayowanufaisha
Msimu huu Bodi ya ligi imevunja rekodi kwa kuifanya Simba kuwa na michezo zaidi ya 10 ya viporo sababu ikielezwa ni kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa
Lakini kila mwaka kuna timu zinashiriki michuano hiyo na haikuwahi kutokea timu hizo zikarundikiwa michezo mingi kama ilivyo kwa Simba msimu huu
Msimu ambao Simba iligoma kucheza ilikuwa ikishinikiza vilabu vya Yanga na Azam Fc vicheze michezo yao mitatu ya viporo!
Mazingira haya yanaifanya ligi ikose msisimko, na haishangazi kuona hakuna mdhamini aliyejitokeza kuidhamini mpaka sasa
Pia ligi imekumbwa na changamoro kubwa ya waamuzi. Kuna maamuzi ya 'hovyo' sana yametawala msimu huu
Ni vyema TFF ikajipanga mapema kuhakikisha inawaandaa waamuzi wake kabla ya msimu mpya.
Haitoshi kuwapa adhabu waamuzi 'wanaoboronga', kwani maamuzi yao yanakuwa tayari yameziathiri baadhi ya timu
TFF ni vyema ikajiridhisha na uwezo wa waamuzi mapema kabla ya kuwatumia kwenya ligi