Kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' Emmanuel Amunike amesema wamejiandaa vya kutosha kuikabili Uganda leo
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Amunike amesema wanafahamu umuhimu wa mchezo huo, ushindi ndio matokeo pekee ambayo yataipa nafasi ya kusonga mbele Stars
"Tumefanya maandalizi ya kutosha, jambo jema ni kwamba wachezaji wote tulionao kambini wako timamu kiafya," alisema Amunike
"Tumefanya kazi kubwa kujiweka tayari, lakini pia tumepitia michezo yetu iliyopita. Kwangu mimi ni muhimu kufanya hivyo ili kujitathmini na kubaini ni maboresho gani unapaswa kufanya"
"Tunafahamu tunacheza na Uganda ambayo tayari imeshafuzu, lakini haimaanishi kuwa mchezo utakuwa mwepesi"
"Uganda wamekuja nchini kulinda heshima ya nchi yao, lakini sisi tuna nafasi ya kuwa miongoni mwa timu zilizofuzu kwa ajili ya fainali za michuano hiyo"
"Tunapaswa kujiamini, tuuchukulie mchezo huo kwa umuhimu mkubwa ili tuweze kushinda. Tuko tayari, naamini wachezaji watafanya kile tulichowaelekeza na kuweza kushinda"