Baada ya Yanga kupoteza mchezo dhidi ya Lipuli Fc kwa kuchapwa bao 1-0, baadhi ya mashabiki wamemshukia kocha Mwinyi Zahera kuwa ndiye chanzo cha timu hiyo kufungwa kwa kutosafiri na timu kwenda mkoani Iringa
Zahera aliondoka jijini Dar es salaam juzi Jumapili na msafara wa timu ya Vita Club ambayo ilikuja kucheza na Simba mchezo wa ligi ya mabingwa
Kaimu Mwenyekiti wa Yanga Samwel Lukumay ametoa ufafanuzi juu ya sababu iliyopelekea Zahera asisafiri na Yanga kwenda mkoani Iringa
Lukumay amesema kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba baina ya Yanga na Zahera, kocha huyo anaruhusiwa kuondoka Yanga wakati wowote anapohitajika kwenda kutimiza majukumu ya timu ya Taifa
"Tulimchukua Zahera huku tukifahamu yeye ni kocha Msaidizi wa timu ya Taifa ya Congo. Hivyo tulikubaliana ataruhusiwa kuondoka kutumikia timu yake ya Taifa wakati wowote atakapohitajika," amesema Lukumay
"Tulimruhusu tangu Ijumaa kwani alitakiwa kuripoti kambi ya timu ya Taifa siku ya Jumapili, isingewezekana kwake kwenda Iringa kisha arudi aende Congo"
Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya viongozi wa Simba walikuwa wakimtuhumu Zahera kuihujumu timu hiyo wakidai hakwenda Congo kama alivyoaga badala yake amekuwa akiambatana na viongozi wa AS Vita.
Hata hivyo Zahera alipuuza tuhuma hizo akisisitiza kuwa anayo haki ya kwenda kuwasalimia maafisa wa AS Vita kwani miongoni mwao wako mabosi wake
"Kocha AS Vita ndiye kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Congo, mimi namsaidia yeye. Mkuu wa Msafara wa AS Vita ndiye Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Congo ambaye ndiye aliyeniajiri mimi katika timu ya Taifa. Lakini pia AS Vita ina wachezaji wannne kwenye kikosi cha timu ya Taifa ambao mimi napaswa kufanya nazo kazi," alisema Zahera
"Kufanya kazi Tanzania hakuninyimi haki ya kutimiza majukumu mengine ya nchi yangu ya Congo"
Zahera anatarajiwa kurejea nchini baada ya mchezo wa kusaka tiketi ya kutinga fainali za AFCON 2019 kati ya Congo dhidi ya Liberia utakaopigwa March 25 huko Congo