Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera ameeleza kushangazwa na kauli zilizotolewa na Msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara aliyemtuhumu kuwa amebaki jijini Dar es salaam ili kuihujumu Simba ambayo leo itachuana na AS Vita Club
Zahera ambaye ni kocha Msaidizi wa timu ya Taifa ya DR Congo, amesema hii sio mara ya kwanza kumsikia Manara akizungumza vitu vya 'hovyo' kuhusu yeye
Akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari jana, Manara alidai wanafahamu Zahera amebaki jijini Dar es salaam kuipokea AS Vita na amekuwa akiambatana na viongozi wa timu hiyo
Zahera amemtaka Manara afahamu kuwa katika msafara wa AS Vita wako watu ambao anafanya nao kazi
"Mimi ni Mkongomani, mimi ni mwalimu wa timu ya Taifa , AS Vita ina wachezaji wanne timu ya Taifa," amesema Zahera
"Kocha mkuu wa AS Vita ni kocha mwenzangu timu ya Taifa, Kiongozi wa msafara wa AS Vita ndiye kiongozi wa shirikisho la soka Congo ambalo ndio wameniajiri timu ya taifa hivyo ni kiongozi wangu.
"Huyo Manara kwa akili yake haoni umuhimu wa mimi kwenda kuwasalimia? eti kisa nimeajiriwa Tanzania. Kipi ninachoweza kukichezesha ama kupanga nikiwa karibu yao?," alihoji Zahera
Kuhusu kutosafiri na timu Iringa Zahera amesema timu ya Taifa ya DR Congo inaingia kambini kesho Jumapili na yeye anapaswa kuwa nchini Congo kesho.