Kwa mara ya kwanza Mzambia Obrey Chirwa alitua nchini Tanzania msimu wa 2015/16 akitokea klabu ya Platinum Fc, usajili wake ukifanikishwa na aliyekuwa kocha wa Yanga wakati huo Hans van Der Pluijm
Chirwa alitua Yanga kuungana na Donald Ngoma na Thabani Kamusoko ambao walitua Yanga miezi sita kabla yake wakitokea klabu hiyo hiyo ya Platinum Fc
Kama ilivyo kwa wachezaji wengi wageni, Chirwa hakuwa na mwanzo mzuri kunako klabu ya Yanga. Lakini mashabiki walimvumilia
Msimu uliofuta Chirwa alikuwa mshambuliaji tegemeo wa kikosi cha Yanga ambapo yeye, Amisi Tambwe na Saimon Msuva waliisaidia Yanga kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu 2016/17
Msimu uliopita ulikuwa mgumu kwa Yanga ambayo ilikumbwa na changamoto za kiuchumi baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti na Mfadhili wake Yusufu Manji
Chirwa alishindwa kuwa mvumilivu na kuamua kuikacha Yanga ambapo alitimkia Misri kujiunga na timu ya daraja la pili
Hata hivyo nako alishindwa ambapo mwishoni mwa mwaka jana wakati wa usajili wa dirisha dogo Chirwa alirejea nchini na kuomba asajiliwe na Yanga
Lakini kutokana na matukio yake ya migomo aliyofanya msimu uliopita, kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera aligoma kuidhinisha usajili wake hivyo akaamua kwenda kuungana na Hans van Pluijm aliyekuwa kocha wa Azam Fc ambaye ndiye aliyemleta nchini
Hata hivyo baada ya Azam Fc kumtimua Pluijm, inaelezwa Obrey Chirwa hana furaha Azam Fc na kwa mara nyingine ameomba kurudi Yanga
Juzi kocha Zahera kwenye moja ya mahojiano yake alifichua kuwa Chirwa amekuwa akiwaambia rafiki zake kuwa anatamani kurudi kuichezea Yanga kwa mara nyingine
Ni dhahiri Chirwa baada ya kucheza Yanga na baadae kuondoka, amebaini hakupata mafanikio huko alikokwenda
Wakati mwingine ni bora kuwa na uvumilivu. Kwa sasa anaona jinsi wachezaji wa Yanga walivyo na furaha licha ya timu kuwa na changamoto kadhaa.
Upendo na sapoti wanayopata wachezaji kutoka kwa mashabiki ni kitu cha kipekee ambacho thamani yake itaendelea kubaki akilini mwao kwa muda mrefu