Katibu Mipango wa zamani wa klabu ya Yanga Abdul Sauko amesema kocha Mkuu wa timu hiyo Mwinyi Zahera amewapa furaha mashabiki wa Yanga katika kipindi ambacho walikuwa wameshakata tamaa na timu yao
Sauko amesema hakuna aliyetarajia kama Yanga ingeweza kushindana na Simba msimu huu katika kuwania ubingwa kutokana na hali mbaya ya kiuchumi inayoikabili timu hiyo
Aidha Sauko amemsifu Zahera kuwa licha ya kukutana na changamoto za ukata ambazo makocha wengi huzikimbia, yeye aliamua kubaki na kujitolea kuwa sehemu ya kupata suluhu
Sauko amesema kocha huyo muwazi na mwenye msimamo, amefanikiwa kutokana na tabia yake hiyo ya kusema ukweli na kusimamia kile anachokiamini kwa gharama yoyote
"Kama Zahera angekosa msimamo ingekuwa ngumu kwa Yanga kuendelea kuwepo kwenye mstari wake. Kuna mambo mengi yanaendelea kwa sasa ikiwemo uchaguzi na ukata, lakini Zahera amesimamia kile anachokiamini katika taaluma yake na hajakubali kuyumbishwa", Sauko amenukuliwa na Mwanaspoti
"Zahera ni mbunifu ndio maana amefungua akaunti ya benki kwa ajili ya wadau kuchangia timu, yote ni kuhakikisha mambo yanakwenda sawa"
Pia Sauko amemsifu kocha huyo kuwa hajatengeneza makundi kwenye timu na kudai amewafanya wachezaji wote kuwa sawa na kujenga nidhamu na umoja.
"Hakuna kitu kizuri kama wachezaji kujengwa akili kuwa, wapo sawa na wote ni muhimu kwa klabu, hakuna mtu muhimu kuzidi wengine"