Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Jerry Muro jana alikuwepo uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha kushuhudia mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara kati ya African Lyon dhidi ya Simba
Katika mchezo huo, Muro aliyewahi kuwa Msemaji wa Yanga alivalishwa jezi ya Simba na msemaji wa timu hiyo Haji Manara

Hata hivyo maoni aliyotoa baada ya mchezo huo ndio yaliyowashangaza wadau wa Yanga hasa ikizingatiwa Muro anafahamika kuwa ni mwanafamilia wa Yanga
Muro alikosoa usajili wa wachezaji Mrisho Ngasa na Haruna Moshi ambao yeye anaamini umri wao umewatupa mkono na hawapaswi kuendelea kucheza mpira
Pia alimkosoa kocha Mwinyi Zahera kuwa hana uwezo wa kuipa mafanikio Yanga, kazi anayoiweza yeye ni kuhamisha mashabiki kuichangia timu
Hata hivyo maoni yake hayafuti ukweli kuwa Yanga inapita katika kipindi kigumu kutokana na ukosefu wa fedha baada ya aliyekuwa Mfadhili na Mwenyekiti wake Yusufu Manji kupata matatizo yaliyopelekea ajiondoe kwenye uongozi wa Yanga
Muro alipata bahati ya kufanya kazi Yanga wakati huo ikiwa na Manji. Lakini mazingira ya wakati huo ni tofauti sana na ya sasa
Usajili wa wachezaji anaowakosoa ulifanikishwa na watu wenye mapenzi ya kweli na Yanga kwani ni hao waliotoa fedha zao kuwezesha usajili huo. Yanga haikuwa na fedha za kufanya usajili mkubwa.
Hakuna Mwana Yanga asiyefahamu mchango wa kocha Mwinyi Zahera kwa timu leo.
Pengine asingekuwa Zahera msimu huu Yanga ingekuwa ikipigania isiteremke daraja
Zahera alikabidhiwa timu ikiwa na wachezaji nane wenye mikataba. Baadhi ya wachezaji walikuwa mbioni kuondoka kutokana na ukata uliokuwa ukiikabili timu
Lakini Zahera kwa kushirikiana na viongozi wa Yanga waliwashawishi wachezaji hao waendelee kubaki.
Wachezaji wengi walisajiliwa kwa ahadi kutokana na ushawishi wake Zahera. Wachezaji kama Heritier Makambo na Klaus Kindoki wamekuwa wakicheza Yanga licha ya kuwa hawakuwa wamelipwa fedha za usajili.
Wapo wachezaji wengi ambao mpaka leo bado wana madai ya fedha za usajili lakini wamekuwa wakijitoa kuipigania timu ili kuwapa furaha mashabiki
Licha ya kukabili na changamoto nyingi, Zahera ameiwezesha Yanga kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi
Hawa akina Ngasa wamekuwa na mchango mkubwa kwa mafanikio iliyopata Yanga mpaka sasa. Ngasa amefunga mabao manne kwenye ligi
Lakini jambo jingine ni kuwa Zahera wakati mwingine anatumia fedha zake za mfukoni kuhakikisha mambo yanakwenda.
Kocha huyo halipwi na Yanga na mwenyewe ameikubali hali hiyo kwa kuwa anafahamu ugumu inayopita Yanga wakati huu
Mafanikio ya Yanga inapaswa yaletwe na Wana Yanga wenyewe. Kulalamika tu hakusaidii. Ndio maana ikaanzishwa kampeni ya kuichangia timu ili kuhakikisha msimu ujao inafanya usajili mzuri na kuboresha maslahi ya wachezaji wake
Nyakati zimebadilika, Yanga sasa haina Manji wala tajiri mmoja wa kumtegemea. Ni umoja wa Wana Yanga wote utakaoleta mafanikio.