Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema timu yake ilikosa ubunifu hasa katika eneo la ushambuliaji na kupelekea kupoteza mchezo dhidi ya Simba jana
Zahera alisema wapinzani wao walikuwa bora lakini anaamini Yanga ingeweza kufanya vizuri zaidi kama wachezaji wake wangekuwa wabunifu kila walipopeleka mashambulizi langoni kwa Simba
Akizungumzia mabadiliko aliyofanya kwenye kipindi cha pili Zahera alisema yaliipunguza kasi Simba na waliweza kutawala mchezo ingawa Simba walirejea mchezoni baadae na kutumia nafasi waliyopata
"Wenzetu wana timu nzuri ushindi waliopata unaakisi ubora wao," alisema Zahera
"Lakini wachezaji wangu walikosa ubunifu hasa katika kushambulia kwani mashambulizi yetu hayakuwa yakifika mwisho"
"Nililazimika kufanya mabadiliko ya kiuchezaji kwenye kipindi cha pili baada ya kubaini Simba walikuwa wakimtumia sana beki wao wa kulia ambaye alikuwa huru kupanda katika kipindi cha kwanza"
"Mabadiliko hayo yalitusaidia sana hasa mwanzoni mwa kipindi cha pili kwani tuliweza kuwadhibiti wapinzani wetu ingawa baadae walitumia nafasi waliyopata kufunga bao"