Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema kikosi chake kinaendelea na mazoezi mkoani Morogoro kujiandaa na mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Simba.
Mchezo huo utapigwa Jumamosi, Februari 16 katika uwanja wa Taifa
Huo utakuwa mchezo wa duru ya pili timu hizo zikiwa zimetoka suluhu ya bila kufungana kwenye mchezo wa kwanza
Tofauti na wengi wanavyouchukulia mchezo huo, Zahera amesema kwake hauna tofauti na michezo mingine.
"Tuko vizuri maandalizi yameendelea vizuri, wachezaji wote 28 wamefanya mazoezi vizuri morali ya wachezaji ni nzuri tokea tuliporudi Tanga. Isipokuwa Kamusoko ndio alikua na matatizo kidogo ya nyama za mguu," Zahera ameuambia mtandao wa Shaffih Dauda
"Jana tulifanya mazoezi na leo tuliendelea na kazi ya technical, tactical na jinsi ya kushambulia, kesho tunaendelea na kazi ya jinsi ya kujilinda."
"Hatuna presha, mechi ya Simba tunajitayarisha kama mechi ya Coastal Union, JKT Tanzania, Singida United na wengine wote. Tofauti na mechi nyingine tumekaa kambini siku mbili halafu mechi ya Simba tunakaa kambini kwa siku tano."
"Mchezo wa mpira wa miguu una matokeo yasiyotabirika. Siyo sawa na hesabu ya kusema 1+1=2, mpira sio kwa sababu ulimfunga X, basi utamfunga Y, hapana Jumapili sio Jumatatu.”
"Kama majina ya siku yako tofauti na timu za mpira duniani kote zipo tofauti. Al Ahly sio Yanga na Yanga sio Al Ahly," amesema
"Mechi dhidi ya Simba ni mechi kama nyingine yoyote, tunacheza na Simba ambao walisema tangu mwanzo wa msimu kwamba wao watabeba ubingwa lakini sisi Yanga mlisikia mwanzo wa ligi tunasema sisi tunacheza ligi mwaka huu ili kubeba ubingwa?"
"Sasa kwa sababu gani mechi hii tuwe na presha? Sisi hatuna presha yoyote, ni wao ndio wana presha. Sisi tukishinda ni furaha, tukitoka sare ni furaha tukifungwa haibadirishi chochote kwenye malengo yetu ya mwaka huu."
Baada ya kumaliza mchezo dhidi ya JKT Tanzania Februari 10, Yanga ilielekea mkoani Morogoro leo ikiwa katika siku ya pili ya maandalizi yake ya siku tano
Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kurejea jijini Dar es salaam keshokutwa Ijumaa, tayari kwa mchezo huo wa 'kukata na shoka'