Beki wa zamani wa Yanga mkongwe Bakari Malima 'Jembe Ulaya' amesema mchezo wa watani wa jadi kati ya Yanga dhidi ya Simba utakaopigwa Jumamosi hii, Februari 16 katika uwanja wa Taifa hautakuwa mwepesi na timu itakayokuwa imejipanga vizuri ndio itakayoweza kuibuka na ushindi
Baada ya ushindi wa Simba wa bao 1-0 dhidi ya Al Ahly jana, mashabiki wa timu hiyo wameongeza tambo wakiamini timu yao itaibuka na ushindi mnono kwenye mchezo huo ambao matokeo yake yatachangia hesabu za ubingwa kwa timu itakayoshinda
Hata hivyo Malima amesema mchezo wa watani wa jadi una presha ya aina tofauti kabisa na michezo mingine hivyo ushindi dhidi ya Al Ahly hauwapi Simba urahisi wa kushinda mchezo dhidi ya Yanga
"Unajua mechi hizi za watani wa jadi huwa hazitabiriki kirahisi kama wengi wanavyodhania. Ushindi wa Simba dhidi ya Al Ahly hautoi taswira kuwa watapata matokeo mbele ya Yanga Jumamosi. Naamini Yanga inaweza kuonyesha maajabu," Malima alinukuliwa na Redio One jana
Yanga imejichimbia mkoani Morogoro ikijifua kujiandaa na mchezo huo utakaopigwa Jumamosi ukitarajiwa kuanza saa 11 jioni
Matokeo ya ushindi kwa Yanga yataiwashia Simba taa nyekundu kuelekea ubingwa wa ligi kuu msimu wa 2018/19 licha ya timu hiyo kuwa na ''furushi' la michezo ya viporo