Msimu huu Yanga imedhamiria hasa kurejea 'anga za Kimataifa' kwa kutwaa taji la ligi au kombe la Shirikisho la Azam (ASFC)
Mpaka sasa mahesabu ya mabingwa hao wa kihistoria yako salama wakiwa wanaongoza ligi kwa tofauti ya alama saba dhidi ya Azam Fc na pia wametinga hatua ya 16 bora ya kombe la FA wakisubiri kuchuana na Namungo Fc
Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera tayari ameandaa mkakati wa kukisuka kikosi chake upya ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika michuano ya CAF msimu ujao iwapo watapata moja ya tiketi mbili
Aidha vipigo inavyoshushiwa Simba katika michuano hiyo, vimemgutusha kocha Zahera ambaye amefanikiwa kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi akiwa na kikosi cha Yanga ambacho mwanzoni mwa msimu kilionekana kama kisingefua dafu msimu huu
Tayari kampeni ya kuwataka Wana Yanga waichangie timu yao imezinduliwa ambapo wadau wametakiwa kuichangia timu hiyo angalau Tsh 2,500/- kila mwezi
Inaelezwa fedha hizo zitatumika kufanya usajili wa wachezaji wapya pamoja na kulipa mishahara
Pia fedha hizo zitaiwezesha Yanga kumaliza ukarabati wa uwanja wake pamoja na kununua vifaa vya kisasa kwa ajili ya mazoezi ya timu
Zahera amepania kuzitumia vyema nafasi 10 za wachezaji 'maproo' ili kukiimarisha kikosi chake
Habari njema ni kwamba mikataba ya wachezaji 'maproo' wa Yanga ukiondoa Heritier Makambo inamalizika mwishoni mwa msimu
Hivyo Yanga itakuwa na nafasi ya kufanya uamuzi sahihi juu ya hatma za wachezaji ambao mikataba yao itakuwa imemalizika bila ya kuingia gharama za ziada