Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera sasa amekuwa sehemu ya familia ya mabingwa hao wa kihistoria kwani ameamua kuhusika moja kwa moja kutatua matatizo ya kiuchumi ya timu hiyo
Ni nadra sana kwa mtu aliyeajiriwa kama kocha kujitoa kama anavyofanya Zahera. Kwa kawaida makocha huwa wanaingia 'mitini' mambo yanapoharibika
Lakini sio Zahera, tena zipo nyakati hutumia hela yake kuisaidia timu hiyo pale mambo yanayoshindikana kabisa
Mpango aliobuni wa kuwashirikisha wadau wa Yanga kuiendesha klabu hiyo utaweza kufanikiwa na kuipaisha Yanga
Mpango huo ambao utamtaka kila Mwana Yanga kuichangia timu hiyo angalau Tsh 2,500 kwa mwezi utaifanya timu hiyo ijiendeshe bila kutegemea mfuko wa mtu mmoja
Yanga ina mashabiki karibu Mil 20 lakini kama wakipatikana Wana Yanga Milioni tano tu wakachangia pesa hiyo, kila mwezi Yanga itakuwa na uhakika wa kuingiza benki zaidi ya Bil 12 na Milioni 500!
Michango ya mwezi mmoja tu itatosha kulipa mishahara ya wachezaji kwa mwaka mzima huku timu hiyo ikiwa na uhakika wa kujiendesha bila kusubiri fedha za wahisani
Zahera tayari amesimamia kufunguliwa kwa akaunti maalum katika benki ya CRDB ambapo kuhakikisha fedha hizo hazichezewi na wajanja, kutakuwa na watia saini watatu, yeye Zahera, nahodha Ibrahim Ajib na Mratibu Hafidh Saleh
Zahera ameanza kwa kuchangia Mil moja na amewataka wadau wa Yanga kuwa tayari kuchangia kadiri ya uwezo wao, kiwango cha Tsh 2,500 kiwe ni cha chini
Wana Yanga wanayokila sababu ya kujivunia uwepo wa kocha huyu. Ingawa haitakuwa mara ya kwanza kwa utaratibu huo kuletwa mbele yao, lakini awali haukuwa umepata mtu sahihi wa kuusimamia kuhakikisha malengo yanafikiwa kama sasa
Tayari matangazo ya redio na TV yameandaliwa kinachosubiriwa ni uzinduzi tu na jambo la kufurahishwa ni kuwa Wana Yanga wengi wameonyesha kuwa tayari kuichangia timu yao kuhakikisha inafanikisha malengo hayo