Kumekuwa na sintofahamu juu ya hatma ya uchaguzi wa Yanga wa kujaza nafasi zilizowazi ambao awali ulipangwa kufanyika Januari 13 ukashindikana kutokana na kesi zilizofunguliwa Mahakamani
Kesi hizo zilifunguliwa na baadhi ya Wanachama wa Yanga dhidi ya Mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi ya TFF na Bodi ya Wadhamini wa Yanga wakipinga mwenendo wa mchakato wa uchaguzi huo kuwa unakwenda kinyume na Katiba ya Yanga
Serikali imesema jitihada zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika mwezi wa pili
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Yusufu Singo amesema Serikali ingependa kuona uchaguzi huo unafanyika mwezi wa pili hivyo jitihada zinafanyika ili kumaliza kesi zilizofunguliwa Mahakamani
“Tulikuwa kwenye harakati za kumaliza kesi kadhaa zilizofunguliwa kuhusu uchaguzi, lakini asilimia kubwa tumezimaliza, imebaki kesi moja ya kupinga kadi za benki kutumika kwenye uchaguzi", Singo amenukuliwa na Mwanaspoti
“Kesi hiyo ndio inatuchelewesha tunapambana kuifuta kwa kufuata hoja zote za waliofungua kesi hiyo, kubwa ni kuhakikisha tunamaliza mapema kabla ya Februari, ili uchaguzi huo ufanyike ndani ya mwezi huo kama ilivyopangwa awali klabu hiyo kuziba nafasi zilizo wazi”