Yanga imeondoshwa katika michuano ya Sportpesa Cup baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Kariobang Sharks ya Kenya
Licha ya kuanza mchezo huo kwa kasi, Yanga ilijikuta ikiwa nyuma kwa mabao 2-0 wakati wa mapumziko. K Sharks ikifunga mabao yake kupitia kwa Duke Abuya na George Abege waliotumia vyema makosa ya safu ya ulinzi ya Yanga
Yanga ingeweza kufunga bao kwenye dakika ya kwanza kabisa lakini kinara wake wa mabao Heritier Makambo alipiga mpira nje akiwa ana kwa ana na mlinda lango wa K Sharks

Katika kipindi cha kwanza mpango wa kocha Mwinyi Zahera haukufanikiwa na akalazimika kufanya mabadiliko wakati wa mapumziko kwa kuwatoa Haruna Moshi na Abdallah Shaibu na kuwaingiza Amissi Tambwe na Thabani Kamusoko aliyeongeza kasi ya mashambulizi ya Yanga kwenye kipindi cha pili
Kukosekana kwa umakini ndiko kulikoinyima Yanga ushindi kwenye mchezo wa leo kwani ilitawala mchezo kwa muda wote wa kipindi cha pili na kutengeneza nafasi nyingi za mabao wakati Sharks ilitumia mashambulizi ya kushitukiza

Bao la kwanza la Yanga lilipatikana kwenye dakika ya 86 likifungwa na Amissi Tambwe aliyetumia makosa ya mlinzi wa K Sharks
Wakati Yanga ikisaka bao la kusawazisha kwenye dakika za majeruhi, ilijikuta ikiruhusu bao la tatu baada ya kiungo Papi Kabamba Tshishimbi kunyang'anywa mpira katika eneo la hatari katika tukio ambalo ilidhaniwa Tshishimbi alifanyiwa madhambi. Abege akaifungia K Sharks bao la tatu.
Baada ya kukosa nafasi mbili za wazi, Makambo alisawazisha makosa yake kwenye dakika za nyongeza alipoifungia Yanga bao la pili akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Ibrahim Ajib
Mlinda lango wa K Sharks nusura aharibu mchezo huo wakati alipojaribu kuwazuia wachezaji wa Yanga wasiuchukue mpira baada ya kufunga bao la pili. Vurugu ziliibuka zikihusisha wachezaji wa timu zote.
Hata hivyo baada ya vurugu hizo kutulia mchezo huo uliendelea lakini Yanga haikufanikiwa kutumia mda mfupi uliokuwa umebaki kusawazisha
Yanga imeungana na Singida United kuyaaga mashindano hayo na kuziacha Bandari Fc na K Sharks zikitinga nusu fainali