Ni dhahiri mlinda lango Beno Kakolanya anaweza asirejee tena Yanga baada ya Mwanasheria wake kuitaka klabu ya Yanga ivunje mkataba wake
Hivi karibuni Mwanasheria huo Leonard Richard alikutana na uongozi wa Yanga akiitaka klabu hiyo ijibu kwa maandishi juu ya maombi ya kuvunjwa kwa mkataba wa mteja wake
Kakolanya hajaichezea Yanga tangu mwishoni mwa mwezi Novemba 2018 baada ya kugoma akishinikiza alipwe malimbikizo ya mishahara na fedha za usajili
Mgomo huo ulimkera Kocha Mwinyi Zahera ambapo licha ya mlinda lango huyo kulipiwa sehemu ya fedha zake za usajili na mdau wa Yanga Cyprian Musiba, Zahera aligoma kumrejesha kikosini akipinga utaratibu uliotumiwa na Musiba kuwa ungeweza kukigawa kikosi chake.
"Niliomba kukutana na Kaya(Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga) namshukuru Mungu maombi yangu yalikubaliwa na nilikaa meza moja naye na kuzungumzia ishu ya mteja wangu Beno.
"Kikubwa kilikuwa ni kuomba wamuachie huru mchezaji huyo kwa maandishi ili aweze kutafuta maisha mengine ya kimpira kutokana na kutegemea suala hilo pekee," Mwanasheria wa Kakolanya amenukuliwa na Mwanaspoti
"Kakolanya anategemea kipaji chake, kitendo cha kuendelea kukaa nje ya majukumu bila ya kuwa na timu nyingine yoyote kinakwamisha maendeleo yake ikiwa ni pamoja na kupoteza kipaji chake ambacho ndiyo kinamuingizia fedha."