Yanga imekuwa na mafanikio makubwa msimu huu kutokana na ushirikiano uliopo kati ya benchi la ufundi, wachezaji, viongozi na mashabiki wa timu hiyo.
Aidha kocha Mwinyi Zahera amekuwa 'chachu' ya mafanikio hayo akifanikiwa kuwatuliza wachezaji na kuwafanya wajitoe kwa moyo wote licha ya kukabiliwa na changamoto za kiuchumi.
Yanga ilitarajiwa kufanya uchaguzi wa kuwapata viongozi wa kuziba nafasi zilizoachwa na waliojiuzulu, lakini uchaguzi huo umeota mbawa baada ya baadhi ya wanachama kufungua kesi Mahakamani kupinga kufanyika kwake
Uchaguzi huo ambao ulikuwa ufanyike kesho Jan 13 kwa kusimamiwa na TFF ikishirikiana na Kamati ya Utendaji ya Yanga , umepingwa na wanachama hao wanaohoji uhalali wa usimamizi wa TFF
Wanachama wengine wanahoji Katiba inayopaswa kutumiwa kati ya ile ya mwaka 1968 na ya 2010.
Wakati TFF ikisubiri maamuzi ya Mahakama juu ya mashauri yaliyofunguliwa ili itangaze hatma ya uchaguzi huo, ni vyema Wana Yanga wakahakikisha mgogoro huo hauvurugi mwenendo mzuri wa timu yao.
Kocha Zahera, wachezaji na benchi la Ufundi wameipigania timu na kuipa mafanikio mpaka sasa licha ya kukabiliwa na mazingira magumu.
Migogoro hii isije ikarudisha nyuma juhudi hizo zilizofanyika badala yake ni vyema ukatafutwa ufumbuzi wa haraka ili kuhakikisha mwenendo wa timu hauathiriki
Kwani migogoro inaweza ikawakatisha tamaa hata wale wanaojitoa kwa ajili ya timu kwa kuona wakati wao wanafanya jitihada, wapo wanaokwamisha juhudi zao
Wakati huu inafaa Wana Yanga wakawa makini sana kuepuka migogoro inayoweza kuwavuruga hasa baada ya timu kuonyesha dalilli njema za kurejesha ubingwa wa ligi kuu Jangwani
Wapinzani wa Yanga wanaweza wakatumia migogoro hii kujinufaisha na kuhakikisha timu haifikii malengo yake
Suala la uchaguzi wa Yanga ni vyema likapatiwa ufumbuzi mapema, ili kuhakikisha timu hiyo inakuwa na uongozi uliokamilika ili kuweza kutatua changamoto zilizopo