Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia Mwenyekiti wake wa Kamati ya Uchaguzi Malangwe Mchungahela, limetangaza kusimamisha uchaguzi wa Yanga uliokuwa ufanyike keshokutwa Jumapili Januari 13 2019 kufuatia baadhi ya Wanachama wa klabu ya Yanga kufungua kesi Mahakamani kupinga uchaguzi huo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo, Mchungahela amesema Wanachama wa Yanga wamefungua kesi za kupinga uchaguzi mikoa ya Dar es salaam, Dodoma, Morogoro, Mbeya na sehemu nyinginezo.
Amesema kuepuka mgongano na mhimili wa Mahakama, TFF imesitisha uchaguzi huo ikisubiri kupokea Maagizo ya Mahakama kulingana na maamuzi yaliyotolewa kufuatia kesi hizo zilizofunguliwa na Wanachama wa Yanga.
Mchungahela amesema TFF itatoa msimamo rasmi juu ya hatma ya uchaguzi huo siku ya Jumatatu, Januari 14 2019
