Licha ya kuondoshwa mapema kwenye michuano ya kombe la Mapinduzi, uongozi wa klabu ya Yanga umewapongeza wachezaji wake vijana walioshiriki michuano hiyo kwa kuonyesha ukomavu
Meneja wa Yanga Nadir Haroub amesema licha ya wachezaji wao wengi kukosa uzoefu, lakini wamejituma na kuipigania timu katika michezo yote mitatu waliyocheza mpaka sasa.
Nadir amesema timu hiyo itaendelea na utaratibu huu wa kuwapa nafasi vijana kwenye michuano mbalimbali ili kuwakomaza kwa manufaa ya baadae ya Yanga
"Tunawapongeza Malindi Fc kwa kupata ushindi kwenye mchezo wa leo (jana) lakini pia nawapongeza vijana wangu kwa kuweza kuonyesha kiwango kizuri," amesema Nadir
"Sisi tumekuja kushiriki mashindano haya na kikosi cha vijana kwa lengo la kuwapa wachezaji wetu uzoefu. Tumebakiwa na mchezo mmoja wa kukamilisha ratiba. Tutaendelea kuwapa nafasi vijana"
Yanga imeondoshwa katika michuano ya kombe la Mapinduzi baada ya kufungwa jana. Matokeo ya mchezo mmoja uliobaki hayawezi kubadili chochote mustakabali wa Yanga kundi B