Uamuzi wa kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera akumvua unahodha mkongwe Kelvin Yondani na kumpa Ibrahim Ajib umetafsiriwa tofauti na baadhi ya wadau wa soka nchini.
Wapo wanaokosoa uamuzi huo wa Zahera wakidai tukio hilo linaweza kuivuruga Yanga hasa ikitokea Yondani hatafurahishwa na uamuzi huo wa kocha
Lakini ukweli ni kwamba mabadiliko ya nahodha wa timu hufanywa mara kwa mara na makocha kadiri wanavyoona inafaa.
Kocha ndiye huwa na wachezaji kwa muda mwingi, hivyo mabadiliko anayofanya ni ili kukidhi yale masuala anayoona ni muhimu
Kwa kawaida nahodha ndiye kiongozi wa wachezaji wenzake ndani na nje ya uwanja. Huyu anakuwa na jukumu kubwa zaidi awapo uwanjani.
Anapaswa kuwa mfano na kuwaongoza wenzake katika kuhakikisha timu inapata matokeo.
Uamuzi wa kumteua Ajib kuwa nahodha wa Yanga ni sahihi sana kwa wakati huu.
Ajib amekuwa chachu ya ushindi katika kikosi cha Yanga, akihusika kutengeneza karibu nusu ya mabao ya Yanga msimu huu.
Zahera amenukuliwa na baadhi ya magazeti ya leo akisema Ajib amekuwa mchazaji mfano kwa wenzake. Amesema mchezaji huyo amebadilika sana na alimpongeza kwa kufanyia kazi mapungufu yake ambayo alikuwa akimkosoa mara kwa mara.
Yondani ni mchezaji mkongwe na naamini hawezi kuvurugwa na mabadiliko haya. Awapuuze wale wanaojaribu kumchonganisha na wachezaji wengine baada ya kuvuliwa unahodha, nafasi aliyoitumikia kuanzia mwanzo wa msimu huu.