Vinara wa ligi kuu ya Tanzania Bara Yanga wameanza vyema michuano ya kombe la Mapinduzi baada ya kuwachapa vinara wenzao wa ligi kuu ya Zanzibar KVZ kwa bao 1-0 katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Amaan Alhamisi usiku.
Yanga ikitumia idadi kubwa ya wachezaji wa kikosi cha vijana, ilijipatia bao la ushindi kwenye dakika ya 75 likifungwa na Shaban Mohammed.
Mohammed alipachika bao hilo baada ya kumalizia pasi murua ya Matheo Anthony aliyewahadaa walinzi wa KVZ kabla ya kutoa pasi kwa mfungaji
Kwenye mchezo huo kiungo wa Yanga Gustava Simon alikuwa kivutio kwa kuonyesha uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, kupiga pasi na uwezo binafsi wa kuchezea mpira
Ushindi huo umeipeleka Yanga kileleni mwa msimamo wa kundi B baada ya kufikisha alama tatu.
Yanga itashuka tena dimbani keshokutwa Jumamosi kuchuana na Azam Fc.