Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera leo anatarajiwa kuzungumza na wachezaji wa zamani waliowahi kuitumikia Yanga katika kikao maalum kilichoitishwa na wakongwe hao.
Mbali ya kuwepo ajenda ya kumpongeza Zahera kwa kazi nzuri, wakongwe hao huenda wakaliibua suala la mlinda lango Beno Kakolanya ambaye Mcongoman huyo ameweka msimamo kuwa hayuko tayari kufanya nae kazi
Jana Zahera aliliambia gazeti la Mwanaspoti kuwa kama kikao hicho kitahusisha ajenda ya Beno, basi yeye hatakuwa tayari kushiriki.
"Kwa kila mwanachama au shabiki wa Yanga ambaye anatamani kuonana na mimi nikiwa na nafasi hawezi kupata tabu nipo tayari kukaa na viongozi, mashabiki, wanachama wa Yanga kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya timu lakini siwezi kupokea magroup au watu wowote wanaotaka kuzungumza na mimi kuhusiana na ishu ya Beno"
"Nimeulizwa mengi kwamba katika kikao changu cha kesho(leo) nitaweza kumsamehe Beno naomba nitolee ufafanuzi hili kama yatazungumzwa hayo basi icho kikao hakiwezi kuchukua ata dakika tano kitakuwa kimeisha," alisema Zahera.
Mapema mwezi huu Zahera aliuambia uongozi wa Yanga uachane na mlinda lango huyo au kama ni lazima kuwa nae kikosini basi yeye ndiye atakayeondoka.
Beno alijitoa katika kikosi cha Yanga mwezi uliopita akishinikiza alipwe malimbikizo ya fedha zake za usajili kiasi cha Tsh Mil 15. Inaelezwa Beno aliondoka kambini usiku wakati kikosi cha Yanga kikijiandaa na mchezo wa ligi dhidi ya Ndanda Fc.
Wakati akiendelea na mgomo, alijitokeza mdau wa Yanga Cyprian Musiba aliyejitolea kumlipia Beno deni lake ambapo alimtangulizia kiasi cha Tsh Mil 2 na kuahidi kumalizia kiasi kilichobaki kwa makubaliano maalum.
Tukio hilo lilimkera zaidi Zahera ambaye alitahadharisha lingeweza kuvuruga utulivu katika kikosi chake kwani Beno hakuwa mchezaji pekee aliyekuwa ana madai. Aliwataka wale wanaotaka kulipa madeni ya wachezaji wafanye hivyo kwa wachezaji wote na sio mchezaji mmoja mmoja