Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera tayari ameondoka nchini Ufaransa kuwahi safari ya kikosi cha Yanga kinachotarajia kuondoka kesho Alhamisi kwenda mkoani Mbeya kwa ajili ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mbeya City.
Yanga inatarajiwa kuondoka kwa usafiri wa ndege shukrani zimuendee Zahera ambaye amewahamasisha mashabiki wa timu hiyo kuichangia timu ili usafiri wa Ndege uweze kupatikana.
Aidha mwenyewe ameahidi kuongeza fedha kama kutakuwa na mapungufu.
Mcongomani huyo anatarajiwa kuwasili leo Jumatano saa nane mchana.
Uhumimu wa mchezo dhidi ya Mbeya City
Yanga imebakiwa na michezo miwili ili kukamilisha duru ya kwanza ya ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu.
Baada ya mchezo dhidi ya Mbeya City, mchezo unaofuata ni dhidi ya Azam FC. Michezo yote Yanga itakuwa ugenini ingawa mchezo dhidi ya Azam Fc utapigwa kwenye uwanja wa Taifa.
Ikiwa inaongoza ligi baada ya kushuka dimbani mara 17 bila ya kupoteza mchezo, kipaumbele cha kwanza ni kuhakikisha mabingwa hao wa kihistoria wanamaliza duru ya kwanza bila ya kuharibu rekodi hiyo.
Zahera anataka timu yake ipate matokeo kwenye michezo yote miwili iliyobaki kukamilisha duru ya kwanza.
Lakini pia michezo dhidi ya Mbeya City inayopigwa katika dimba lao mara nyingi sio rahisi.
Kumbukumbu za msimu uliopita mchezo dhidi ya Mbeya City uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 uligubikwa na vurugu zisizo za kawaida.
Katika mchezo huo Jeshi la Polisi lililazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatuliza mashabiki wa timu hiyo waliokuwa wakimrushia mawe mlinda lango Youthe Rostand wakati mchezo ukiendelea.
Kuna wakati Rostand alilazimika kulikimbia lango kunusuru maisha yake kutokana na vurugu za mashabiki hao.
Pia ni katika mchezo huo ambao licha ya mchezaji wa Mbeya City kutolewa nje kwa kadi nyekundu, timu hiyo ilimaliza mchezo ikiwa na wachezaji 11! Aliyekuwa kocha Msaidizi wa Yanga wakati huo Shedrack Nsajigwa analikumbuka vizuri tukio hili.
Ni aina ya mchezo ambao washindani wa Yanga watapenda kuona Yanga haipati alama zote tatu ili wapate 'ahueni' kutokana na vinara hao wa ligi kuongoza kwa tofauti ya alama nyingi.
Hata hivyo uwepo wa kocha Mwinyi Zahera kwenye benchi la Ufundi, utaongeza mara dufu kasi ya Yanga na kama ilivyokuwa mchezo dhidi ya Tanzania Prisons, Zahera amepania kuchukua alama zote tatu kwenye mchezo huo.