Vinara wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Yanga wameanza vyema michuano ya kombe la FA baada ya kuifumua Tukuyu Stars mabao 4-0 katika mchezo wa raundi ya tatu uliopigwa leo uwanja wa Taifa.
Mabao matatu 'hat-trik' yaliyofungwa na Amisi Tambwe na moja la Heritier Makambo yameihakikishia Yanga kufuzu kwenda raundi ya nne ya michuano hiyo katika mchezo ambao Yanga ilitawala kwa muda.


Tambwe alifunga mabao yake katika dakika za 13, 35 na 55 wakati Makambo alifunga bao la nne kwenye dakika ya 80.
Yanga ingeweza kufunga mabao zaidi kwenye mchezo huo kama sio uimara wa mlinda lango wa Tukuyu Stars New Afrika.

Kiungo Haruna Moshi 'Boban' aliyetua Yanga kwenye dirisha dogo la usajili akitokea klabu ya African Lyon amecheza mchezo wake wa kwanza hata hivyo alidumu dimbani kwa dakika 28 tu baada ya kupata majeraha na nafasi yake kuchukuliwa na Deus Kaseke.

Katika muda mfupi aliokuwa dimbani 'Boban' alionyesha uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kupiga pasi za uhakika.