Mabingwa wa kihistoria wa soka Tanzania Yanga leo wanashuka kwenye uwanja wa Taifa kuikabili Tukuyu Stars katika mchezo wa kombe la FA (ASFC), raundi ya tatu.
Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na rekodi ya kipekee msimu huu ambapo inaongoza ligi kuu ya Tanzania Bara ikiwa imeshuka dimbani mara 17 na kujikusanyia alama 47.
Imeshinda michezo 15 na kutoka sare michezo miwili huku timu hiyo ikiongoza kwa kupachika mabao.
Katika kujihakikishia inacheza michuano ya Kimataifa msimu ujao, uongozi wa Yanga umesema hauachi kitu msimu huu, sio ligi wala kombe la FA.
Mratibu wa kikosi cha Yanga Hafidh Saleh amesema wamejiandaa kikamilifu kuelekea mchezo huo ambao ushindi utaipeleka Yanga raundi ya nne.
Katika mchezo huo mashabiki wa Yanga huenda wakamshuhudia kwa mara ya kwanza kiungo mpya wa timu hiyo Haruna Moshi 'Boban' ambaye tayari ameidhinishwa kuwatumikia vinara hao wa ligi kuu akitokea klabu ya African Lyon.