Vuta ni kuvute baina ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) na Klabu ya Yanga kuhusu nani asimamie uchaguzi wa kujaza nafasi zilizo wazi imefika tamati baada ya Yanga kukubali yaishe.
Awali, Yanga walikuwa wanagoma uchaguzi wao kuwa chini ya TFF kwa kudai hawatendewi haki, lakini hivi sasa wamekubali jambo hilo lifanyike na uchaguzi uishe kwa usalama bila shida yoyote baada ya kufanya vikao mfululizo na Serikali.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Yanga, Samuel Lukumay, aliliambia Mwanaspoti kuwa uchaguzi wao utafanyika kama kawaida baada ya kufikia makubaliano ya pamoja baina yao, Serikali na TFF.
Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Januari 13 mwakani na tayari wagombea walifanyiwa usaili chini ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF inayoongozwa na Mwenyekiti, Ally Nchungahela na sasa wanasubiri hukumu ya wagombea wawili waliokata rufaa kupinga kuenguliwa kwao.
"Uchaguzi utafanyika kama kawaida na hivi sasa tupo hapa TFF kwaajili ya kuzungumza baadhi ya mambo, tumeafikiana vizuri kwahiyo kila kitu kitaenda sawa," alisema Lukumay.
Msuguano baina ya TFF na Yanga kuhusu uchaguzi kwamba nani ana haki ya kusimamia ulimalizwa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe baada ya kukutana mara kadhaa na pande hizo mbili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa utulivu wa hali ya juu.