Fadlu aichambua MC Alger, aweka mkakati wa ushindi

Shabiki NambaMoja By Shabiki NambaMoja
β€’
1h ago
Fadlu aichambua MC Alger, aweka mkakati wa ushindi

POINTI tatu, soka la kushambulia na umakini mkubwa katika kuzuia mashambulizi ya kushtukiza ya wapinzani ndiyo hesabu za Kocha Mkuu wa Yanga, Fadlu Davids, kuelekea mchezo dhidi ya MC Alger ya Algeria katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL).

Yanga itawakaribisha mabingwa hao wa Algeria kesho Jumamosi, Novemba 28, 2026, kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar, katika mchezo wa kwanza wa Kundi B.

Akizungumza na waandishi wa habari leo kuelekea mtanange huo, Fadlu amesema anatambua ukubwa wa changamoto inayowakabili, lakini anaamini ubora wa kikosi chake unawapa nafasi nzuri ya kuanza kampeni yao kwa ushindi.

Kocha huyo raia wa Afrika Kusini amesisitiza kuwa licha ya Yanga kuwa na ndoto kubwa za kufika mbali katika michuano hiyo, kwa sasa akili na nguvu zao zote zimeelekezwa katika kuhakikisha wanavuna pointi tatu dhidi ya MC Alger.

“Kucheza nyumbani katika mchezo wa ufunguzi ni fursa nzuri ya kuanza mashindano kwa matokeo mazuri. Lengo letu ni kupata pointi zote tatu. Tunawaheshimu wapinzani wetu na tunafahamu uwezo wao, lakini pia tuna imani na ubora wa kikosi chetu,” amesema Fadlu.

AMESOMA MBINU ZA MC ALGER

Fadlu amefichua kuwa benchi lake la ufundi limefanya kazi ya kuwachambua kwa kina wapinzani wao, likitilia mkazo mabadiliko ya kiufundi yaliyotokea kufuatia mabadiliko ya kocha katika kikosi cha MC Alger.

Miongoni mwa michezo ambayo Fadlu na wasaidizi wake wameitumia kuwasoma wapinzani hao ni ule wa hivi karibuni dhidi ya JS Kabylie katika Ligi Kuu ya Algeria.

“Tumekuwa tukiifuatilia na kuichambua timu pinzani, ikiwemo mchezo wao wa hivi karibuni dhidi ya JS Kabylie. Kwa kuwa wana kocha mpya, kuna baadhi ya mabadiliko ya kiufundi ambayo tumeyaona, hivyo tunatarajia kukutana na timu yenye mbinu tofauti.”

Hata hivyo, Fadlu amesema pamoja na kuwafahamu wapinzani wao, kipaumbele chake kikubwa ni kukiboresha kikosi chake na kuhakikisha kinatumia ipasavyo maeneo ambayo yanaweza kuwapa faida katika mashambulizi.

KUSHAMBULIA KWA TAHADHARI

Ingawa falsafa ya Fadlu ni kucheza soka la kushambulia, kocha huyo ameweka wazi kuwa hataki kuona wachezaji wake wakipoteza uwiano kati ya kushambulia na kulinda lango lao.

Anatambua kuwa kupeleka idadi kubwa ya wachezaji mbele kunaweza kuacha mianya ambayo MC Alger inaweza kuitumia kupitia mashambulizi ya kushtukiza.

Fadlu amesema kuruhusu bao kunaweza kubadilisha kabisa sura ya mchezo, hasa iwapo wapinzani wataamua kujilinda zaidi na kutumia mbinu za kuvuruga mwendelezo wa mchezo.

“Tunataka kucheza kwa mtazamo wa kushambulia na kutafuta ushindi, lakini pia tunapaswa kuwa makini katika namna tunavyosawazisha majukumu ya kushambulia na kulinda lango letu.”

Fadlu anataka kuona Yanga ikicheza kwa ujasiri, lakini kwa nidhamu kubwa ya kiufundi ili kuepuka makosa yanayoweza kuwagharimu Wananchi.

KIKOSI KAMILI CHAMPA NGUVU

Jambo jingine linalompa matumaini Fadlu kuelekea pambano hilo ni kupata fursa ya kufanya kazi na kikosi chake kizima baada ya mapumziko ya michezo ya kimataifa.

Kocha huyo amesema kipindi hicho ni muhimu katika kujenga muunganiko wa timu, kufanya uchambuzi wa video na kuhakikisha wachezaji wanakuwa katika hali nzuri kimwili, kiakili na kisaikolojia.

“Sisi ni mabingwa wa Tanzania tuna kikosi kizuri, benchi imara la ufundi na malengo makubwa. Tuna imani na uwezo wetu.”

Fadlu amesisitiza kuwa ushindani mkubwa uliopo katika Ligi ya Mabingwa Afrika unahitaji kila mchezo kupewa uzito wake, huku maandalizi bora yakiwa msingi wa kupata matokeo yanayotarajiwa.

POINTI TISA ZA NYUMBANI

Katika hesabu zake za kuivusha Yanga hatua ya makundi, Fadlu ameendelea kusisitiza umuhimu wa kushinda michezo yote mitatu ya nyumbani, jambo litakalowaweka Wananchi katika mazingira mazuri ya kusaka tiketi ya robo fainali.

“Ni muhimu sana kuanza mashindano kwa ushindi, hasa tunapocheza nyumbani. Lengo letu ni kupata pointi zote tatu katika michezo yetu ya nyumbani.”

Pambano la kesho pia linabeba kumbukumbu chungu kwa Wananchi baada ya MC Alger kuwanyima nafasi ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo misimu miwili iliyopita.

Wakati huo, Yanga ilikubali kipigo cha mabao 2-0 nchini Algeria kabla ya kulazimishwa sare tasa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, licha ya kuhitaji ushindi ili kusonga mbele.

Safari hii, Fadlu ana nafasi ya kuandika ukurasa mpya dhidi ya wababe hao wa Algeria.

Yanga SC Stories

Aziz Ki awapa ujumbe mashabiki Yanga 'tutapambana'
Aziz Ki awapa ujumbe mashabiki Yanga 'tutapambana'
1h ago
READ MORE β†’
Wananchi wajitokeza kuchangia damu Viwanja vya Maturembeta Zanzibar
Wananchi wajitokeza kuchangia damu Viwanja vya Maturembeta Zanzibar
3h ago
READ MORE β†’
Tuko tayari kuikabili MC Alger - Job
Tuko tayari kuikabili MC Alger - Job
4h ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Ijumaa, Novemba 27 2026
Magazeti ya leo Ijumaa, Novemba 27 2026
8h ago
READ MORE β†’
Yanga yakamilisha maandalizi New Amaan Complex tayari kuikabili MC Alger
Yanga yakamilisha maandalizi New Amaan Complex tayari kuikabili MC Alger
19h ago
READ MORE β†’
Aziz Ki aweka ahadi, apania ligi ya mabingwa
Aziz Ki aweka ahadi, apania ligi ya mabingwa
1d ago
READ MORE β†’
CAFCL msimu huu VAR kuanza kutumika hatua ya makundi
CAFCL msimu huu VAR kuanza kutumika hatua ya makundi
1d ago
READ MORE β†’
Yanga ilivyojifua New Amaan Complex, Zanzibar
Yanga ilivyojifua New Amaan Complex, Zanzibar
1d ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Alhamisi, Novemba 26 2026
Magazeti ya leo Alhamisi, Novemba 26 2026
1d ago
READ MORE β†’
Tom Ambongile kuziamua Yanga na MC Alger CAFCL
Tom Ambongile kuziamua Yanga na MC Alger CAFCL
1d ago
READ MORE β†’