Aziz Ki aweka ahadi, apania ligi ya mabingwa

Shabiki NambaMoja By Shabiki NambaMoja
β€’
38m ago
Aziz Ki aweka ahadi, apania ligi ya mabingwa

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki, ameweka wazi dhamira yake ya kuendelea kuipa mafanikio klabu hiyo, akisisitiza kuwa kurejea kwake Jangwani kuna malengo makubwa mawili; kuendeleza utawala wa mataji ya ndani na kuifikisha timu mbali katika michuano ya kimataifa.

Nyota huyo raia wa Burkina Faso, ambaye amerejea Yanga msimu huu wa 2026/27 baada ya kupitia Wydad Casablanca ya Morocco na Al-Ittihad SC ya Libya, amesema anatambua ukubwa wa matarajio ya mashabiki kutokana na imani kubwa waliyonayo kwake.

Aziz Ki amefunguka kuhusu safari yake ya maisha ya soka, sababu za kurejea Yanga, ushindani wa ubingwa dhidi ya Simba pamoja na malengo yao katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

MWANZO WA SAFARI YA KIMATAIFA

Baada ya Yanga kujenga utawala wake katika mashindano ya ndani, Aziz Ki anaamini wakati umefika kwa Wananchi kuonyesha ukubwa wao katika anga za kimataifa.

Kiungo huyo haridhishwi na mwenendo wa Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa misimu miwili iliyopita, akiamini ubora wa kikosi walichonacho unawapa nafasi ya kufanya makubwa zaidi.

“Kwa misimu miwili mfululizo tumeishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, hii sio nzuri kwetu kutokana na aina ya wachezaji bora tulionao, licha pia ya ushindani mkubwa unaoonyeshwa na washindani wetu,” anasema Aziz Ki.

Kauli hiyo inakuja wakati Yanga ikijiandaa kufungua pazia la hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya MC Alger ya Algeria, Jumamosi, Novemba 28, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar.

Kwa Aziz Ki na wenzake, kuvuka hatua ya makundi msimu huu ni moja ya changamoto kubwa wanazopaswa kuzishinda ili kukidhi matarajio ya mashabiki wao.

AKIRI KUONDOKA YANGA ULIKUWA UAMUZI MGUMU

Aziz Ki amekiri kuwa uamuzi wa kuondoka Yanga Juni 2025 na kujiunga na Wydad Casablanca ulikuwa miongoni mwa maamuzi magumu katika maisha yake ya soka.

Ingawa alikuwa na dhamira ya kujipima katika mazingira mapya yenye ushindani mkubwa, mapenzi yake kwa Yanga hayakutoweka.

“Kila mchezaji ana ndoto ya kujaribu changamoto mpya na hasa katika Ligi zenye ushindani mkubwa ikiwemo za Kaskazini mwa Afrika, nilitaka kujipima uwezo wangu nje ya eneo nililolizoea, ingawa moyo na mapenzi yangu yalibakia Yanga,” anasema.

Safari yake kupitia Morocco na Libya imempa uzoefu mpya, huku akiyachukulia mambo ambayo hayakwenda vizuri katika klabu hizo kuwa sehemu ya mafunzo yanayomjenga mchezaji.

Anasema kurejea kwake Yanga kumempa fursa nyingine ya kuitumikia klabu anayoipenda na kulipa imani kubwa aliyoonyeshwa na viongozi pamoja na mashabiki.

KUENDELEZA MAKALI YAKE YA PASI ZA MABAO

Pamoja na kujijengea umaarufu kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao, Aziz Ki ameweka wazi kuwa mafanikio ya timu ndiyo anayoyapa kipaumbele kuliko takwimu zake binafsi.

Kiungo huyo amesema jukumu lake kubwa ni kutengeneza nafasi za mabao kwa wachezaji wenzake na kuhakikisha kunakuwa na muunganiko mzuri katika uchezaji wa timu.

“Mchezaji yeyote anaweza kufunga ikitokea hiyo nafasi kwa sababu sio suala la mshambuliaji pekee, nimekuwa nikionyesha uwezo huo mkubwa, ila kipaumbele changu cha kwanza ni kutoa asisti na kutengeneza muunganiko mzuri,” anasema Aziz Ki.

Mbali na majukumu yake ya kiufundi, nyota huyo amekuwa akionyesha sifa za uongozi kwa kuwahamasisha wachezaji wenzake ndani na nje ya uwanja.

Anasema tabia hiyo inatokana na dhamira yake ya kuhakikisha kila mchezaji anatambua wajibu wake katika kuipigania nembo ya Yanga na kutimiza malengo ya klabu.

ATIA NENO MABADILIKO YA BENCHI LA UFUNDI

Akizungumzia mabadiliko ya benchi la ufundi yaliyoshuhudia kuondoka kwa Manqoba Mngqithi na kurejea kwa Fadlu Davids, Aziz Ki amesema anaheshimu falsafa na mchango wa kila mmoja wa makocha hao.

Hata hivyo, anaamini ujio wa Fadlu unatoa nafasi kwa kikosi hicho kujipanga upya, kuweka kando changamoto zilizopita na kuelekeza nguvu katika kutimiza malengo ya msimu huu.

“Ni furaha kwangu kufundishwa na makocha wote wawili, naheshimu mchango wa kila mmoja wao kwa sababu lengo lilikuwa ni kupata kile kilichokuwa bora, ila kusema kimbinu ni nani bora zaidi ya mwenzake hilo siwezi kwa kweli,” anasema.

AHADI KWA WANANCHI

Aziz Ki, aliyejiunga na Yanga kwa mara ya kwanza Julai 15, 2022, akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast, anatambua kuwa mashabiki wanatamani kumuona akirejesha makali aliyokuwa nayo kabla ya kuondoka.

Hilo amelichukulia kama jukumu kubwa na ameahidi kuendelea kupambana ili kulinda imani waliyonayo kwake.

“Kurejea kwangu tena Yanga ni fahari kutokana na imani kubwa niliyopewa na viongozi, hii inaonyesha malengo ya timu na mwelekeo wetu kiujumla, nitaendelea kupambana na kuendeleza imani ya mashabiki wanaoendelea kuniunga mkono,” anasema.

Aziz Ki ameweka bayana kurejea Jangwani si suala la mapenzi pekee, bali ni dhamira ya kuendeleza historia ya mafanikio aliyowahi kuiandika akiwa na jezi ya kijani na njano.

Kutetea mataji ya ndani, kuendeleza ushindani na kuivusha Yanga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ndiyo malengo yanayomkabili nyota huyo msimu huu.

Mtihani mkubwa wa kutimiza malengo hayo ya kimataifa unaanza Jumamosi hii dhidi ya MC Alger, visiwani Zanzibar.

Yanga SC Stories

CAFCL msimu huu VAR kuanza kutumika hatua ya makundi
CAFCL msimu huu VAR kuanza kutumika hatua ya makundi
3h ago
READ MORE β†’
Yanga ilivyojifua New Amaan Complex, Zanzibar
Yanga ilivyojifua New Amaan Complex, Zanzibar
4h ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Alhamisi, Novemba 26 2026
Magazeti ya leo Alhamisi, Novemba 26 2026
8h ago
READ MORE β†’
Tom Ambongile kuziamua Yanga na MC Alger CAFCL
Tom Ambongile kuziamua Yanga na MC Alger CAFCL
18h ago
READ MORE β†’
Kamwe afanya hamasa Zanzibar kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya MC Alger
Kamwe afanya hamasa Zanzibar kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya MC Alger
21h ago
READ MORE β†’
Hatma ya majeraha ya Maxi kufahamika baada ya wiki nne
Hatma ya majeraha ya Maxi kufahamika baada ya wiki nne
1d ago
READ MORE β†’
Awamu ya pili ya maandalizi ya kuikabili MC Alger
Awamu ya pili ya maandalizi ya kuikabili MC Alger
1d ago
READ MORE β†’
MC Alger watua mapema kuikabili Yanga
MC Alger watua mapema kuikabili Yanga
1d ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Jumatano, Novemba 25 2026
Magazeti ya leo Jumatano, Novemba 25 2026
1d ago
READ MORE β†’
Bobosi katika rada za Yanga
Bobosi katika rada za Yanga
1d ago
READ MORE β†’