Mwamuzi wa kimataifa kutoka Afrika Kusini, Tom Abongile, ndiye atakayekuwa na jukumu la kupuliza filimbi katika mchezo wa kukata na shoka kati ya Yanga na MC Alger ya Algeria, katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL).
Mtanange huo wa kwanza wa Kundi B utapigwa Jumamosi, Novemba 28, 2026, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar, huku kila timu ikihitaji kuanza kampeni yake kwa matokeo mazuri.
Abongile atakuwa na jukumu la kusimamia sheria 17 za mchezo wa soka katika pambano hilo linalotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na historia ya timu hizo katika michuano ya kimataifa.
MCHEZO WENYE HISTORIA YA KISASI
Pambano hilo linabeba kumbukumbu chungu kwa Wananchi baada ya MC Alger kuwanyima nafasi ya kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika misimu miwili iliyopita.
Wakati huo, Yanga ilikubali kipigo cha mabao 2-0 nchini Algeria kabla ya kulazimishwa suluhu ya bila kufungana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, licha ya kuhitaji ushindi ili kusonga mbele.
Safari hii, kikosi cha Kocha Mkuu Fadlu Davids kitakuwa na nafasi nyingine ya kulipa kisasi, huku kikilenga kutumia faida ya kucheza mbele ya mashabiki wake kuvuna pointi tatu.