Hersi afunguka ujenzi wa uwanja, Serikali yatoa mwongozo

Shabiki NambaMoja By Shabiki NambaMoja
β€’
2d ago
Hersi afunguka ujenzi wa uwanja, Serikali yatoa mwongozo

Rais wa Yanga SC, Injinia Hersi Said, ametoa ufafanuzi wa kina kuhusu hatua iliyofikiwa katika mradi wa kihistoria wa ujenzi wa uwanja wa klabu hiyo, akibainisha kuwa Kamati ya Utendaji na Baraza la Wadhamini zimekubaliana kuendelea na mfumo wa kuhamisha ardhi ya mradi kwenda kwenye kampuni ya Jangwani Complex Limited.

Akizungumza Novemba 18, 2026, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Makao Makuu ya Yanga, Jangwani jijini Dar es Salaam, Hersi amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya kupokea mwongozo kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali.

Hersi ameeleza kuwa Novemba 17, 2026, klabu hiyo ilipokea barua yenye mwongozo rasmi kuhusu njia tatu zinazoweza kutumika katika utekelezaji wa mradi huo, ambapo uongozi umechagua kuendelea na mfumo uliokuwa umependekezwa awali.

YANGA NA GSM KUMILIKI ASILIMIA 50 KILA MMOJA

Katika kufafanua makubaliano ya uwekezaji kati ya Yanga na GSM Group, Hersi amesema klabu hiyo inachangia ardhi, huku GSM ikichangia mtaji wa fedha kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa uwanja.

Kupitia kampuni maalumu ya Jangwani Complex Limited, inayotambulika kitaalamu kama Special Purpose Vehicle (SPV), Yanga itamiliki asilimia 50 ya hisa, huku GSM Group ikimiliki asilimia 50 zilizobaki.

“Kwa hiyo, tuliona ni muhimu kuunganisha rasilimali za pande zote mbili ili kupata mradi mkubwa ambao ungenufaisha klabu na mwekezaji,” amesema Hersi.

Amefafanua kuwa mfumo huo unalenga kuhakikisha maslahi ya wanachama wa Yanga yanalindwa sambamba na usalama wa fedha zitakazowekezwa na GSM.

SAFARI ILIANZA JANUARI 7

Hersi amewakumbusha wanachama kuwa mchakato wa kutafuta mwekezaji wa ujenzi wa uwanja ulianza rasmi Januari 7, 2026, baada ya klabu kutoa tangazo la kutafuta mshirika wa utekelezaji wa mradi huo.

Baada ya kupitia maombi yaliyowasilishwa na taasisi mbalimbali, Februari 2, 2026, Kamati ya Utendaji iliyokutana Zanzibar ilitangaza GSM Group kuwa mshirika rasmi wa Yanga katika mradi huo.

Hatua hiyo ilifuatiwa na majadiliano ya kina kuhusu muundo wa uwekezaji, wajibu wa kila upande na namna ya kulinda maslahi ya klabu.

Juni 9, 2026, uongozi wa Yanga uliwasilisha makubaliano hayo mbele ya Baraza la Wadhamini katika kikao kilichohudhuriwa pia na Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali.

Miongoni mwa waliohudhuria kikao hicho, kwa mujibu wa Hersi, ni Waziri Mkuu wa sasa, Dk. Mwigulu Nchemba, ambaye alikuwa mjumbe wa Baraza la Wadhamini, pamoja na Anthony Mavunde.

WANACHAMA 877 WALITOA RIDHAA

Katika Mkutano Mkuu wa Yanga uliofanyika Agosti 2, 2026, suala la kuhamisha ardhi ya mradi kutoka katika mfumo wa usimamizi wa Baraza la Wadhamini kwenda Jangwani Complex Limited liliwasilishwa kwa wanachama.

Hersi amesema jumla ya wanachama 877 waliohudhuria mkutano huo walitoa ridhaa ya kuendelea na mchakato huo baada ya kupewa maelezo kuhusu makubaliano ya uwekezaji na mgawanyo wa hisa.

Baada ya kupata ridhaa hiyo, Sekretarieti ya klabu iliwasilisha maombi rasmi kwa Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali, ikiambatanisha nyaraka za umiliki wa ardhi, makubaliano ya uwekezaji, maelezo ya mradi na mihutasari ya vikao mbalimbali vya klabu.

HERSI AELEZA KILICHOCHELEWESHA UJENZI

Akijibu maswali ambayo yamekuwa yakiulizwa na wanachama kuhusu sababu za ujenzi kutokuanza licha ya kutangazwa kwa ushirikiano na GSM, Hersi amesema klabu ilikuwa ikikamilisha taratibu muhimu za kisheria na kiutawala.

“Hatukuweza kusaini makubaliano leo na kesho kuanza kuchimba bila kuhakikisha taratibu zote za umiliki wa ardhi, ridhaa ya wanachama na vibali vinavyohitajika zimekamilika.

“Hii ni mali ya klabu yetu na ni jukumu letu kuhakikisha tunailinda,” amesema Hersi.

Amesisitiza kuwa kuchelewa kuanza kwa ujenzi hakukutokana na kukosekana kwa dhamira ya kutekeleza mradi huo, bali umuhimu wa kuhakikisha mali za klabu zinalindwa kwa manufaa ya wanachama na vizazi vijavyo.

YANGA YACHAGUA NJIA YAKE

Baada ya kupokea mapendekezo matatu kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kamati ya Utendaji na Baraza la Wadhamini zimekubaliana kuendelea na mfumo wa Jangwani Complex Limited.

Hersi amesema mfumo huo utaendana na makubaliano ya wanahisa, yanayojulikana kama Shareholders Agreement (SHA), huku klabu ikizingatia maeneo muhimu yaliyoelekezwa na mamlaka za Serikali kwa ajili ya kulinda maslahi ya pande zote mbili.

Uamuzi huo unaashiria hatua nyingine muhimu katika safari ya Yanga kuelekea utekelezaji wa ndoto yake ya kuwa na uwanja wake.

Yanga SC Stories

Goals : Polisi Tanzania 0-2 Yanga, NBC PL (FT)
Goals : Polisi Tanzania 0-2 Yanga, NBC PL (FT)
10h ago
READ MORE β†’
FT : Polisi Tanzania 0-2 Yanga, NBC PL
FT : Polisi Tanzania 0-2 Yanga, NBC PL
11h ago
READ MORE β†’
Kikosi : JKT Tanzania vs Yanga, NBC PL, Nov 20
Kikosi : JKT Tanzania vs Yanga, NBC PL, Nov 20
14h ago
READ MORE β†’
Mudathir amemaliza adhabu, tayari kurejea kikosini
Mudathir amemaliza adhabu, tayari kurejea kikosini
18h ago
READ MORE β†’
Dladla awaaga Wananchi
Dladla awaaga Wananchi
19h ago
READ MORE β†’
Matchday; Polisi Tanzania vs Yanga, NBC PL, Nov 20
Matchday; Polisi Tanzania vs Yanga, NBC PL, Nov 20
19h ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Ijumaa, Novemba 20 2026
Magazeti ya leo Ijumaa, Novemba 20 2026
22h ago
READ MORE β†’
Yanga yawasili Moshi tayari kuikabili Polisi Tanzania
Yanga yawasili Moshi tayari kuikabili Polisi Tanzania
1d ago
READ MORE β†’
Yanga yakamilisha maandalizi tayari kuifuata Polisi Tanzania
Yanga yakamilisha maandalizi tayari kuifuata Polisi Tanzania
1d ago
READ MORE β†’
Dikgacoi atamba Yanga ipo tayari kuivaa Polisi Tanzania
Dikgacoi atamba Yanga ipo tayari kuivaa Polisi Tanzania
1d ago
READ MORE β†’