Inaelezwa klabu ya FAR Rabat ya Morocco inafikiria kumtoa kwa mkopo kiungo mshambuliaji Allan Okello ikiwa ni miezi sita tu tangu ajiunge na timu hiyo ya Jeshi akitokea klabu ya Yanga.
Okello aliondoka Yanga mwanzoni mwa msimu huu baada ya kung'ara na mabingwa hao wa nchi akifunga mabao 14 na asisti 8 katika mechi 24 za ligi alizocheza.
Hata hivyo tangu atue Morocco amekuwa sio rahisi kwake huku presha ya mashabiki dhidi yake ikiwa kubwa.
Wengi wanamuona kama hamudu mikiki mikiki ya soka la nguvu la Morocco huku wengine wakiweka matumaini kuwa pengine anaweza kuwa bora baadae pale atakapozoea.
Kwa mujibu wa makubaliano kati ya Yanga na AS FAR wakati wa mauziano ya mchezaji huyo, Yanga itapewa nafasi ya kwanza kumsajili mchezaji huyo kama AS FAR wataamua kumuuza au kumtoa kwa mkopo.
Kwa maana yake itakuwa rahisi kwa Yanga kumrejesha kwa mkopo au pengine kumnunua moja kwa moja kama watamuhitaji.
Baada ya Okello kuondoka, Yanga ilimrejesha Stephane Aziz Ki. Hata hivyo bado inaonekana eneo la kiungo cha ushambuliaji bado linahitaji kuongezewa nguvu.
Ni takribani wiki nne zimesalia kuelekea kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili. Upo uwezekano kwa staa boy kurejea tena kwa Wananchi.