Kiungo mkabaji Khalid Aucho aliyewahi kung'ara na kikosi cha Yanga, ameagwa kwa heshima na timu ya taifa ya Uganda, Uganda Cranes, baada ya kumaliza safari yake ya miaka 13 akiitumikia nchi yake katika michuano mbalimbali ya kimataifa.
Nyota huyo aliagwa katika Uwanja wa Hoima City Stadium, wakati Uganda ilipokutana na Botswana katika mchezo wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, Aucho alipewa heshima ya kipekee ambapo wachezaji wa Uganda na Botswana waliunda safu ya heshima (Guard of Honour), huku Rais wa Shirikisho la Soka Uganda (FUFA), Moses Magogo, akimkabidhi zawadi maalumu ya kumbukumbu kutambua mchango wake kwa taifa.
Pamoja na maandalizi ya kumuwezesha Aucho kucheza mchezo wake wa mwisho akiwa na jezi ya Uganda Cranes, kiungo huyo hakupata nafasi ya kuingia uwanjani kutokana na majeraha yaliyomuweka benchi kwa dakika zote za mchezo.
Hata hivyo, hilo halikuzuia shirikisho, wachezaji wenzake na mashabiki kumuenzi kwa mchango wake mkubwa katika timu hiyo kwa zaidi ya muongo mmoja.
Aucho alionekana kuguswa na tukio hilo huku akipokea heshima zilizokuwa zimeandaliwa kwa ajili yake.
Aucho, mwenye umri wa miaka 33, alicheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa Novemba 30, 2013, na katika kipindi chote cha kuitumikia Uganda Cranes alifanikiwa kucheza mechi 77.
Katika safari yake hiyo, alishiriki fainali tatu za AFCON, mwaka 2017, 2019 na 2025, huku akifanikiwa pia kuvaa kitambaa cha unahodha wa timu hiyo.
Miongoni mwa mafanikio makubwa aliyoshiriki ni kuisaidia Uganda kurejea katika fainali za AFCON mwaka 2017 nchini Gabon, baada ya kusubiri kwa miaka 38 bila kushiriki michuano hiyo.