Kiungo mshambuliaji wa Kimataifa wa Uganda Allan Okelloamekuwa na wakati mgumu huko Morocco tangu ajiunge na AS FAR akitokea klabu ya Yanga kwenye dirisha lililopita la usajili.
Okello amekuwa na wakati mgumu kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga Pedro Goncalves. Inaelezwa uongozi wa Yanga unafuatiliwa kwa karibu maendeleo ya nyota huyo.
Ilikuwa ni ahadi ya Rais wa Yanga Injinia Hersi Said ambaye alisema Okello amekwenda Morocco lakini Yanga ni nyumbani na wanaweza kumrejesha wakihitaji kufanya hivyo.
Taarifa za ndani zimebainisha kuwa Okello hafurahii muda mdogo anaopatiwa na klabu hiyo akitamani kurejea kwa waajiri wake wa zamani, Yanga.
Yanga ina nafasi ya kumrejesha Okello hata kwa mkopo pale dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa mwezi ujao.
Ni wazi kwenye dirisha dogo Yanga itahitaji kuongeza nguvu eneo lake la kiungo cha ushambuliaji licha ya urejeo wa Stephane Aziz Ki ambaye ameanza taratibu awamu ya pili ya maisha yake ndani ya Yanga.