Baada ya kuanza majukumu yake, Kocha Mkuu wa Yanga Fadlu Davids ameweka wazi kila mchezaji ana nafasi sawa kwenye kikosi chake na anachohitaji ni wachezaji kujituma na kupambania nafasi zao kwenye uwanja wa mazoezi.
Jana ilikuwa siku ya kwanza kwa Fadlu kuongoza mazoezi visiwani Zanzibar ambapo kikosi cha mabingwa hao wa nchi kimeweka kambi ya siku 10.
Akizungumza muda mfupi baada ya kuwasili Zanzibar, Fadlu alisema licha ya ufinyu wa muda wa maandalizi, ataendelea kukiimarisha kikosi chake kimbinu taratibu lakini jambo muhimu kwa wachezaji ni kupambana akiamini timu hiyo ina wachezaji bora.
Katika maandalizi hayo, Yanga itawakosa wachezaji waliokwenda kwenye majukumu ya timu za Taifa huku baadhi ya wachezaji wakirejea taratibu kutoka kwenye majeraha.
“Tupo tayari kwa kwenda kuanza kazi, tutakuwa na wachezaji ambao hawakwenda kujiunga na timu za taifa, hakuna muda kupoteza zaidi tunatakiwa kuanza maandalizi haraka, changamoto ni moja tu kuna baadhi ya wachezaji ni majeruhi hasa eneo la kiungo lakini tutawaangalia wengin.”
“Hii ni kambi fupi ambayo naweza kusema ni maalumu sana kwa ajili ya wachezaji, natarajia kuona kila mchezaji atapambana kwa kiwango kikubwa, kwa kuwa kila mchezaji aliyepo hapa ni bora, hii ni njia ya kila mmoja kuonyesha ubora wake uwanjani.
“Tutakuwa na hatua kwa hatua katika kuingiza falsafa yertu kwenye timu kitu muhimu hapa ni kutaka kuona mtindo wetu wa uchezaji tunaanza kuushika kwa haraka, tuna wachezaji wazoefu ambao hatutapata shida ya kuwapatia kile tunachotaka wakifanye," alisema
Baada ya mapumziko ya kalenda ya FIFA, Yanga itaanza na Polisi Tanzania mchezo wa ligi kuu utakaopigwa Novemba 20 na kufuatiwa na mchezo dhidi ya Mbeya City kabla ya kuanza kampeni ya hatua ya makundi (CAFCL) nyumbani dhidi ya MC Alger.