Beki wa Yanga SC, Mohammed Hussein ‘Zimbwe Jr’, amesema kikosi hicho hakijaridhishwa na nafasi kilichopo kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, akisisitiza kuwa jukumu lao kubwa kwa sasa ni kuhakikisha wanatetea ubingwa walioutwaa msimu uliopita.
Akizungumza na wanahabari kuelekea mchezo dhidi ya Kagera Sugar utakaopigwa kesho Jumapili katika dimba la KMC Complex, Zimbwe Jr amesema wanafahamu hali ya wapinzani wao na umuhimu wa alama tatu katika mchezo huo.
Hata hivyo, amesema Yanga nayo ina malengo yake ambayo bado haijayafikia, hivyo wachezaji wamejipanga kupambana kuhakikisha wanarejesha timu katika nafasi inayostahili kulingana na hadhi na matarajio ya klabu hiyo.
“Tunafahamu wapinzani wetu wanashika nafasi gani kwenye msimamo wa ligi na wanahitaji nini ili kujinasua katika hali waliyonayo. Hata hivyo, nasi hatujaridhishwa na nafasi tuliyopo kwa sasa, kwani haiendani na malengo yetu.
“Sisi ni mabingwa watetezi, na lengo letu kuu ni kuhakikisha tunautetea ubingwa wetu kwa mafanikio. Hilo ndilo jukumu letu na tutapambana kulitimiza,” amesema Zimbwe Jr.
Katika hatua nyingine, beki huyo amezungumzia changamoto inayoweza kuletwa na benchi la ufundi la Kagera Sugar, akimtaja kocha wa timu hiyo kuwa mwenye uzoefu mkubwa katika soka la Tanzania na anayefahamu baadhi ya mambo kuhusu Yanga kutokana na historia yake ya kuifundisha klabu hiyo.
Hata hivyo, Zimbwe Jr amewatoa hofu mashabiki wa Yanga, akieleza kuwa benchi la ufundi chini ya Simon Dladla limefanya maandalizi ya kutosha, likiwemo zoezi la kuichambua na kuisoma Kagera Sugar kabla ya kukutana uwanjani.
“Kagera Sugar wana kocha mzuri na mwenye uzoefu mkubwa katika ligi yetu. Tunafahamu pia kuwa amewahi kuifundisha Yanga, hivyo kuna baadhi ya mambo kuhusu klabu yetu anayoyafahamu.
“Niwatoe hofu Wananchi kwani tuna benchi jipya la ufundi lenye walimu wapya na mbinu mpya. Tuna imani kubwa na benchi letu la ufundi, kwani tayari wamefanya kazi kubwa ya kuichambua na kuisoma Kagera Sugar,” amesema.