Kocha Mkuu wa Yanga Manqoba Mngqithi amesema bado hajaridhishwa na ufanisi wa safu yake ya ushambuliaji kutokana na matumizi hafifu ya nafasi wanazotengeneza.
Manqoba alitoa kauli hiyo jana baada ya mchezo wa mkondo wa kwanza kuwania kufuzu hatua ya makundi ligi ya mabingwa dhidi ya CFFA ya Madagascar Yanga ikishinda mchezo huo kwa mabao 4-0.
"Tulikuwa na mchezo mzuri, kipindi cha kwanza tulitengeneza nafasi zaidi ya 7 na pengine tulipaswa kumaliza mchezo mapema"
"Lakini naona bado tuna changamoto kubwa kwa wachezaji wetu kwenye eneo la umaliziaji. Hatuwezi kutengenez nafasi nyingi halafu tukashindwa kuzitumia"
"Hili sio jambo zuri kwa sababu zipo mechi hatutatengeneza nafasi nyingi kama hivi na tutapaswa kutumia nafasi hizo chache," alisema Manqoba
Manqoba alibainisha kuwa wakati wa mapumziko alizungumza na wachezaji wake kuongeza utulivu na kupunguza kasi pale wanapofika kwenye lango la CFFA.
Katika dakika 10 za kipindi cha pili Yanga ikafunga mabao matatu ya haraka haraka na kujihakikishia ushindi huo muhimu wa ugenini sasa wakihitaji kumaliza kazi kwenye mchezo wa marudiano ambao watakuwa nyumbani siku ya Jumatano.