Kesho Jumamosi Oktoba 17 pale uwanja wa Azam Complex, mabingwa wa soka Tanzania Bara Yanga watakuwa uwanjani kumenyana na CFFA ya Madagascar kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza kuwania tiketi ya kufuzu hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Afrika (CAFCL).
Huu utakuwa mchezo wa kwanza kwa Yanga tangu watoke kupoteza pambano dhidi ya watani zao Simba kwenye ligi kuu ya NBC.
Kuna ujumbe mahsusi wachezaji wa Yanga wanataka kuwapa mashabiki wao kupitia mchezo huu kuwaonyesha wanayo timu ya kupigania kila taji msimu huu na kilichotokea kwenye mchezo uliopita ni matokeo tu ya mpira wa miguu.
Mashabiki wameendelea kununua tiketi kwa wingi ambapo mpaka sasa tiketi zilizosalia ni Mzunguuko pekee huku VIP A na B zikiwa zimemalizika.
Mchezo dhidi ya CFFA kesho utapigwa mapema saa 9 Alasiri.
