Baada ya kukosekana kwa muda mrefu, mashabiki wa Yanga huenda wakamshuhudia japo kwa dakika chache beki na nahodha msaidizi wa timu hiyo Dickson Job kwenye mchezo unaofuata wa ligi ya mabingwa mkondo wa kwanza kuwania tiketi ya makundi dhidi ya CFFA ya Madagascar.
Job amerejea kikosini kwa wiki kadhaa hata hivyo amekuwa akiendelea na program za kurejesha utimamu wa mwili kabla ya kutumika kwenye mechi za mashindano.
Kwa sasa Job anafanya mazoezi kikamilifu na timu ikiwa ni ishara ya urejeo wake kikosini.
Wanayanga wamekuwa na shauku kubwa kumuona Job akirejea tena kikosini ili kuimarisha safu ya ulinzi ambayo kwenye mchezo uliopita dhidi ya Simba ilionekana kuyumba.
Katika muda wote ambao Job amekosekana, nahodha Bakari Nondo Mwamnyeto na Ibrahim Bacca wameendelea kuwa tegemeo huku wakati mwingine Oumar Komara akianzishwa badala ya Mwamnyeto.
Job na mshambuliaji Clement Mzize walikuwa nje kwa muda mrefu, hata hivyo Mzize tayari ameanza kutumika kwenye mechi za kimashindano akiingia kipindi cha pili kwenye mchezo uliopita dhidi ya Simba.