Wakati Yanga ikijiandaa na mchezo wa ligi kuu dhidi ya watani zao Simba utakaopigwa kesho Jumamosi kwenye uwanja wa Uhuru, maandalizi hayo pia ni pamoja na mechi zitakazofuata baada ya mchezo huo.
Oktoba 17 Yanga itarejea kwenye kampeni ya kusaka tiketi ya hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa (CAFCL) ambapo wataumana na CFFA ya Madagascar.
Mchezo wa kwanza Yanga itakuwa ugenini kabla ya kuhitimisha mchezo wa pili Oktoba 24 kwenye uwanja wa Azam Complex.
Habari njema kwa Wananchi ni kuwa huenda mechi zote mbili zikapigwa uwanja wa Azam Complex.
Madagascar hakuna uwanja uliopitishwa na CAF kutumika kwenye michuano ya ligi ya mabingwa na hivyo klabu hiyo kulazimika kuomba kutumia uwanja wa Azam Complex ambao pia Yanga wanautumia kwenye michuano hiyo.
Inaelezwa tayari klabu hiyo imewasilisha CAF uwanja wa Azam Complex kama uwanja wao wa nyumbani kwa ajili ya mchezo wa kwanza dhidi ya Yanga.
Hatua hiyo itaipa nafasi Yanga kucheza mechi zote mbili hapa hapa nchini na pengine kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kutinga hatua ya makundi.