Mchezo wa ligi kuu ya NBC kati ya Simba dhidi ya Yanga unatarajiwa kupigwa Oktoba 10 kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam, imefahamika.
Licha ya wenyeji wa mchezo huo Simba kutoweka hadharani mapema uwanja waliochagua, lakini imefichuka ni dimba la Uhuru.
Aidha kulikuwa na nafasi pia kwa mchezo huo kupigwa uwanja wa New Amaan Complex kama wenyeji wangechagua uwanja huo ambao umefunguliwa hivi karibuni baada ya kufanyiwa ukarabati.
Kikosi cha Yanga kinaendelea na maandalizi yake kuelekea mchezo huo ambapo Meneja wa habari na Mawasiliano wa mabingwa hao wa nchi Ali Kamwe amesema watakuwa tayari kucheza uwanja wowote ambao wapinzani wao watachagua.
Huo utakuwa mchezo wa pili wa dabi ya Kariakoo msimu huu baada ya timu hizo kukutana kwenye Ngao ya Jamii Yanga ikiibuka na ushindi wa bao 1-0.
Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na rekodi ya kibabe dhidi ya watani zao kwenye ligi kwani katika mechi nane zilizopita, Yanga imeshinda sita na kutoka sare mechi mbili.