Ulimwengu wa soka nchini Tanzania umeingia kwenye simanzi nzito kufuatia kifo cha mwanachama na shabiki nguli wa klabu ya Yanga SC, Haji Omari Ramadhani Mpili, maarufu kama ‘Mzee Mpili’, aliyefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumatatu, Septemba 28, 2026.
Mzee Mpili alifikwa na mauti katika Kituo cha Afya cha Wilaya ya Ikwiriri mkoani Pwani, alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu.
Msemaji wa familia amethibitisha kuwa mwili wa marehemu unatarajiwa kuzikwa leo jioni, majira ya saa 10:00 katika Makaburi ya Msikiti Mkuu wa Ikwiriri.
Huu ni msiba mkubwa kwa klabu ya Yanga, Viongozi wa klabu hiyo, wanachama, mashabiki, wadau na wakazi wa Wilaya ya Ikwiriri watampumzisha gwiji huyo kwenye nyumba yake ya milele.
Alivyotikisa Soka la Bongo
Mzee Mpili atakumbukwa kama mmoja wa mashabiki wenye ushawishi mkubwa kwenye soka la Tanzania katika muongo mmoja uliopita.
Alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na misemo yake ya kipekee, ujasiri wa kuongea na vyombo vya habari, pamoja na matamko yake makali kuelekea mechi za watani wa jadi kati ya Yanga na Simba SC (Dabi ya Kariakoo).
Kauli yake maarufu ya "Sisi tuna watu, hatuwezi kufungwa na Simba" iligeuka kuwa wimbo na kaulimbiu iliyowaunganisha na kuwapa jeuri mashabiki wa Yanga wakati timu yao inapokutana na Simba.
Wakati huo Yanga ilikuwa bado 'haijajipata' hivyo hamasa za kina Mzee Mpili zilichangia kwa kiasi kikubwa kuongeza morali na ari ya timu na kweli Yanga haikukubali kufungwa na Simba licha ya wakati huo 'kutembeza bakuli'.
Klabu ya Yanga SC, kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii, imeelezea masikitiko yake makubwa na kutoa pole kwa familia, ndugu, na wapenzi wote wa soka nchini kwa kuondokewa na mtu aliyetia nakshi ya kipekee kwenye burudani ya soka la ndani.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu Mzee Mpili mahali pema peponi. Amen.