Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, ameendelea kuonyesha wazi dhamira ya klabu hiyo kuwasajili wachezaji wenye viwango bora, akisisitiza kuwa wachezaji wanaoonyesha uwezo mkubwa katika timu pinzani wanajiweka karibu zaidi na kuhamia Yanga.
Hersi amesema anafurahia kuona wachezaji wenye uwezo wakicheza soka la kiwango cha juu, huku akisisitiza kuwa Yanga ni sehemu ambayo mchezaji bora anaweza kutimiza ndoto zake za kisoka.
Akizungumza na Bongo FM, Hersi alisema sifa ya mchezaji kusajiliwa na Yanga ni kiwango kizuri anachokionyesha katika timu yake.
“Kila mchezaji wa timu pinzani anavyoonyesha kiwango bora, ndivyo anavyojiweka karibu na kuja kuitumikia Yanga. Niseme tu, napenda sana kuona wachezaji wote wazuri wakiwa kwenye timu yangu.”
Hersi aliongeza kuwa haoni sababu ya mchezaji mwenye uwezo kutoka ndani ya Tanzania kukataa kujiunga na Yanga, akisisitiza kuwa klabu hiyo ina mvuto kwa wachezaji wa ndani na nje ya nchi.
“Wala sioni mchezaji yoyote hapa Tanzania anayeweza kukataa kuja kucheza Yanga. Iwe mchezaji wa ndani au wa nje. Ndiyo maana karibu wachezaji wote nina namba zao.”
Aidha kuelekea dirisha lijalo la usajili, Injinia Hersi ametoa dokezo kuwa Yanga inaweza kuwa na shughuli kubwa katika kipindi hicho.
Kwa msisitizo, Hersi alisema:
“Nikwambie tu, dirisha dogo kuna watu watauana...! Tuombe uzima.”