Kiungo mshambuliaji wa Yanga Juma Abushiri ‘Chuga Boy’ amekuwa mmoja wa mashujaa wa Ngorongoro Heroes baada ya kufunga bao lililoweka msingi wa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burundi na kuiwezesha Tanzania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 20 (AFCON U-20) mwaka 2027.
Ngorongoro Heroes ilitinga hatua hiyo baada ya kuibuka na ushindi huo katika mchezo wa nusu fainali ya michuano ya CECAFA uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Tanzania iliingia uwanjani ikiwa na lengo moja kubwa, kupata ushindi ambao ungeipa nafasi ya kufikia fainali na wakati huohuo kukata tiketi ya AFCON U-20.
Mwanzo wa mchezo ulionyesha wazi kuwa vijana wa Tanzania walikuwa wamejipanga kwa kazi hiyo. Mashambulizi yalikuwa yakielekezwa mara kwa mara katika lango la Burundi, huku presha ikizidi kuongezeka.
Dakika ya 16, Chuga Boy alifungua ukurasa wa mabao baada ya kuifungia Tanzania bao la kwanza. Bao hilo liliamsha shangwe kubwa Uwanja wa Uhuru na kuwapa wenyeji nguvu zaidi ya kuendelea kusaka bao la pili.

Burundi ilijaribu kujibu, lakini Ngorongoro Heroes iliendelea kuwa na udhibiti wa mchezo na kutengeneza nafasi kadhaa.
Juhudi hizo zilizaa matunda tena dakika ya 33, wakati Faraji Kayanda alipofunga bao la pili na kuifanya Tanzania iingie mapumzikoni ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili kilikuwa na sura tofauti kwa kiasi, kwani Burundi iliongeza mashambulizi ikitafuta mabao ya kurejea mchezoni. Hata hivyo, safu ya ulinzi ya Tanzania haikuyumba.
Abubakar Nizar ‘Ninju’ na wenzake walifanya kazi kubwa kuhakikisha Burundi haipati nafasi rahisi mbele ya lango la Tanzania. Ngorongoro Heroes nayo iliendelea kupambana hadi dakika za mwisho na kulinda faida yake.
Ushindi huo umeifanya Tanzania kufuzu AFCON U-20 pamoja na Sudan, ambayo nayo ilipata nafasi hiyo baada ya kuitoa Uganda kwa ushindi wa mabao 3-2 katika nusu fainali nyingine.
Tmu hizi sasa zitakutana kwenye mchezo wa fainali kumpata bingwa wa CECAFA U20 huku zote zikiwa na tiketi ya kucheza Afcon U20 fainali zitakazofanyika mwaka 2027