Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Alex Ngai, amewashukia watu wanaosambaza taarifa na uvumi kuhusu kocha mkuu wa timu hiyo, Manqoba Mngqithi, akisisitiza kuwa kocha huyo bado yupo imara ndani ya kikosi cha mabingwa hao wa Tanzania.
Ngai amesema kuna watu wanaofanya kampeni na propaganda zinazolenga kuvuruga utulivu wa Yanga kuelekea mchezo mkubwa wa Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba, unaotarajiwa kuchezwa Oktoba 10.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Ngai alidai kuwa baadhi ya watu wameandaliwa kwa ajili ya kusambaza taarifa zinazolenga kumchafua au kumtoa Mngqithi katika klabu hiyo.
“Nilichogundua mnamuogopa mwamba kwa kuwa kasema anautaka ubingwa wa Afrika. Acheni kuzusha na kuandika habari za kipuuzi. Nasikia mmegaiwa iPhone 17 huko mpige propaganda. Huyu yupo, na derby ijayo mnae, na kipigo kiko palepale,” aliandika Ngai
Kauli hiyo imedhihirisha uungwaji mkono wa Mngqithi ndani ya Yanga, kocha huyo akianza msimu kwa matokeo mazuri.
Tangu alipotua Jangwani, Mngqithi amewaongoza mabingwa hao watetezi kushinda mechi zote sita za Ligi Kuu walizocheza, huku pia akifanikiwa kuivusha timu hiyo katika raundi ya kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mbali na matokeo hayo, Mngqithi alitwaa tuzo ya Kocha Bora wa Ligi Kuu kwa mwezi Agosti 2026, jambo linaloonyesha mwanzo mzuri wa safari yake katika soka la Tanzania.