Kocha Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi, ameonesha imani kubwa na uwezo wa kikosi chake, akieleza kuwa timu hiyo ina nafasi ya kufanya makubwa zaidi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwemo kufika hatua ya fainali.
Yanga imeweka malengo ya angalau kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa baada ya kufanikiwa kucheza hatua ya makundi kwa misimu mitatu mfululizo. Hata hivyo, Mngqithi anaamini malengo hayo yanaweza kuwa makubwa zaidi kutokana na ubora na upana wa kikosi alichonacho msimu huu.
Kocha huyo wa zamani wa Mamelodi Sundowns ameeleza kuwa tofauti kubwa na msimu uliopita ni namna Yanga ilivyoboreshwa katika suala la kina cha kikosi.
Amesema uliopita Yanga ilikuwa na kikosi cha kwanza chenye ubora mkubwa, lakini haikuwa na wachezaji wengi wa kutosha walioweza kutoa mchango mkubwa pale walipohitajika.
“Msimu uliopita nilichogundua kuhusu Yanga ni kwamba hawakuwa na kikosi imara kwa upana. Walikuwa na kikosi cha kwanza kizuri sana, lakini zaidi ya hapo kulikuwa na wachezaji watatu au wanne tu ambao kweli wangeweza kuisaidia timu.”
Mngqithi amesema hali hiyo imebadilika msimu huu baada ya Yanga kuongeza ubora na kina cha kikosi, jambo analoliona kuwa ni muhimu katika safari ya timu kwenye michuano mikubwa ya Afrika.
“Msimu huu tumeimarika kuhakikisha tuna wachezaji 24 hadi 26 wenye ubora. Clement na Job wakirudi tuna wachezaji 28 wenye uwezo wa kushindana.”
Akumbuka pambano la Yanga na Sundowns
Mngqithi pia amerejea katika kumbukumbu ya wakati akiwa sehemu ya benchi la ufundi la Mamelodi Sundowns, ambapo timu hiyo iliiondoa Yanga katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.
Kocha huyo anasema Yanga ilikuwa karibu sana kufuzu na kwamba baadhi ya matukio katika mchezo huo yangeweza kubadilisha kabisa historia ya pambano hilo.
“Nakumbuka nilikuwa bado Sundowns wakati tulipoiondoa Yanga kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa. Lakini ukweli ni kwamba walikuwa karibu sana. Hata bao walilofunga lilikuwa na utata fulani kwa sababu lingeweza kuwapeleka nusu fainali.”
Kauli hiyo inaonesha namna Mngqithi anavyotambua uwezo wa Yanga katika michuano ya kimataifa, huku uzoefu wake wa muda mrefu katika mashindano ya Afrika ukimpa picha ya kile kinachohitajika ili timu ifike mbali.
Yanga inalenga kwenda mbali zaidi
Wakati Yanga ikijiandaa kwa mchezo wa marudiano dhidi ya Gaborone United katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa, Mngqithi ana matumaini makubwa kwamba kikosi chake kinaweza kuendelea na safari hiyo na baadaye kushindana dhidi ya vigogo wa soka la Afrika.
Uzoefu wa Mngqithi katika Ligi ya Mabingwa, ukiwemo kutwaa taji akiwa sehemu ya benchi la ufundi la Mamelodi Sundowns, unaweza kuwa moja ya silaha muhimu kwa Yanga katika kutekeleza malengo yake.
Kwa sasa, lengo la kwanza ni kuhakikisha Yanga inavuka hatua ya awali, lakini kauli za Mngqithi zinaashiria kuwa mipango yake haiishii robo fainali.
Kwa kocha huyo, Yanga ya msimu huu ina uwezo wa kuota ndoto kubwa zaidi hadi kufikia hatua ya kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.