Kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga, Pacome Zouzoua, bado anasubiri tuzo ya Mchezaji Bora (MVP) wa msimu wa 2024/25, ambayo anaamini alistahili kuipata iicha ya ukimya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Msimu huo ulikwisha kwa Yanga kutetea ubingwa wao huku Pacome akiwa mhimili mkubwa wa mafanikio hayo. Hadi sasa sherehe za utoaji wa tuzo hizo kwa misimu miwili sasa hazijafanyika, jambo linalozua maswali mengi miongoni mwa wadau wa soka nchini.
Katika msimu huo, raia huyo wa Ivory Coast alionyesha kiwango cha hali ya juu ambapo alifanikiwa kufunga mabao 11 na kutoa pasi 9 akiibeba Yanga kutetea taji la ligi kuu mwa msimu wa nne.
Pacome alifunga bao la kwanza kwenye mchezo wa mwisho kuhitimisha msimu dhidi ya Simba huku akitoa pasi ya bao la pili lililofungwa na Clement Mzize katika mchezo ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Akizungumza jana nyumbani kwake baada ya kutembelewa na Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe, Pacome alitumia nafasi hiyo kuuliza vipi mpaka sasa tuzo hizo hazijatolewa pengine akitarajia wahusika kutoa ufafanuzi juu ya mkwamo uliopo.