Klabu ya soka ya Yanga leo inafungua ukurasa mpya wa kihistoria wakitarajia kusaini mkataba wa ujenzi wa jengo jipya la kisasa la ghorofa 12, linalofahamika kama ‘Yanga Tower’, litakalojengwa katika makutano ya mitaa ya Mafia na Nyamwezi, Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Hafla hiyo kubwa ya utiaji saini inafanyika leo katika eneo hilo ambalo lina historia ya kipekee kwa kuwa ndipo chimbuko rasmi la klabu hiyo kongwe nchini lilipoanzia mwaka 1935.
Jengo hilo la ghorofa 12 linatarajiwa kuwa na miundombinu ya kisasa ikiwemo ofisi za klabu, kumbi za mikutano, maduka ya vifaa vya michezo vya klabu (Yanga Megastore), pamoja na maeneo ya biashara yatakayopangishwa ili kuongeza ukwasi wa kifedha wa klabu hiyo ya Jangwani.
Tayari makazi ya zamani ya klabu hiyo namba 59 yaliyokuwa eneo hilo yamebuliwa na wataalamu wa vipimo wapo kazini ili kuruhusu wakandarasi kuanza kazi mara moja.
Tukio hili linajiri wakati klabu hiyo ikiwa pia kwenye mchakato wa kuelekea ujenzi wa uwanja wake mpya wa kisasa katika eneo la Jangwani.