Klabu ya Yanga imeanza rasmi maandalizi ya ujenzi wa uwanja wake mpya wa kisasa katika eneo la kihistoria la Jangwani jijini Dar es salaam, huku miundombinu ya awali ikianza kuwekwa ili kupisha kazi hiyo kubwa.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, amethibitisha kuwa eneo la Makao Makuu ya Klabu hivi sasa linatayarishwa kwa ujenzi wa majengo ya muda.
Majengo hayo yatatumika kama kambi, makazi, na ofisi za wakandarasi pamoja na wataalamu watakaosimamia mradi huo tangu mwanzo hadi mwisho.
Maandalizi hayo yameanza baada ya kukamilika kwa upatikanaji wa vibali vya ujenzi pamoja na usajili rasmi wa kampuni ya ubia kati ya Yanga na GSM.
Katika mkataba huo wa ushirikiano wa kibiashara, pande zote mbili zitakuwa na umiliki wa ubia wa asilimia 50 kwa 50, ambapo klabu imetoa ardhi na mwekezaji anagharimia ujenzi mzima.
Ujenzi huo wa uwanja unatarajiwa kuchukua kati ya miezi 18 hadi 24 hadi kukamilika kwake. Tayari wataalamu na wakandarasi, wakiwemo wale kutoka nchini Uturuki, wameanza kuonekana katika eneo hilo kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa mwisho wa ardhi na kuanza kazi mara moja.