Mchezo wa ligi ya mabingwa kati ya Gaborone United dhidi ya Yanga unakuja wakati timu hizo zikiwa katika mazingira tofauti kabisa ya ushindani.
Kwa upande mmoja, Gaborone United wanaingia kwenye mchezo wakiwa na faida ya kucheza nyumbani na uzoefu wa kutosha katika soka la Botswana.
Kwa upande mwingine, Yanga wanaonekana kuwa na faida kubwa katika suala la match fitness, kasi ya ushindani na kujiamini.
Ushindani na fomu ya timu
Yanga wanaingia katika mchezo huu wakiwa kwenye mwanzo mzuri wa msimu. Mabingwa hao wa Tanzania Bara tayari wamecheza mechi tano za ligi kuu na kushinda zote, huku wakifunga mabao 15 na kuruhusu mawili pekee. Takwimu hizo zinaonyesha timu yenye uwiano mzuri kati ya uwezo wa kufunga na uimara wa safu ya ulinzi.
Gaborone United, kwa upande wao, ni mabingwa wa Botswana mara mbili mfululizo na walimaliza msimu uliopita kwa alama 74. Hata hivyo, tofauti kubwa ipo kwenye maandalizi ya msimu huu. Wenyeji wamecheza mechi moja tu ya ligi, wakishinda 2-1 dhidi ya Prisons.
Hilo linaweza kuwa panga lenye makali mawili. Upande mmoja, Gaborone wamepata muda wa maandalizi na kurekebisha kikosi; lakini upande mwingine, ukosefu wa mechi nyingi za ushindani unaweza kuwafanya wakose kasi inayohitajika dhidi ya timu ambayo tayari imeingia kwenye rhythm ya ligi.
Mbinu: Gaborone watataka kucheza kwa tahadhari
Gaborone United wanaonekana kufahamu ukubwa wa changamoto iliyo mbele yao. Msemaji wa klabu, Tshepo Molwane, ameeleza kuwa wamekuwa wakiifuatilia Yanga kwa karibu, ikiwa ni pamoja na ushindi wao wa 2-0 dhidi ya Fountain Gate.
Hii inaashiria kwamba Gaborone hawataingia uwanjani bila mpango. Wanatarajiwa kuwa na nidhamu katika ulinzi, kupunguza nafasi kati ya mistari na kutafuta mashambulizi ya kushtukiza pale watakapopata nafasi.
Kwa Yanga, changamoto itakuwa kuvunja ukuta huo bila kupoteza uwiano wa timu. Ikiwa wataongeza wachezaji wengi mbele kwa wakati mmoja, wanaweza kuacha nafasi nyuma ambazo Gaborone wanaweza kuzitumia kupitia counter-attacks.
Mngqithi ana Kazi ya kuepuka mtego wa kujiamini
Kocha wa Yanga, Manqoba Mngqithi, ametoa tahadhari dhidi ya kuidharau Gaborone United. Hili ni jambo muhimu kwa sababu kwenye mashindano ya klabu Afrika, tofauti ya ukubwa wa majina si mara zote huamua matokeo.
Mngqithi amesisitiza maeneo kadhaa ya Gaborone ambayo Yanga wanapaswa kuyaangalia: uwezo wao wa kujilinda, mashambulizi ya kushtukiza na mipira ya kutenga.
Hivyo, Yanga wanahitaji kucheza kwa subira na akili, badala ya kukimbilia kutafuta bao la mapema kwa gharama ya kupoteza shape ya timu.
Shalulile: Silaha inayoweza kubadilisha mchezo
Mchezaji mmoja ambaye macho yatakuwa kwake ni Peter Shalulile. Mshambuliaji huyo ana uzoefu mkubwa wa mashindano ya juu ya Afrika kutokana na muda alioutumia Mamelodi Sundowns.
Uzoefu kama huo unaweza kuwa muhimu sana katika mchezo wa aina hii. Shalulile si tu tishio ndani ya boksi; uwezo wake wa kushambulia nafasi, kukimbia nyuma ya mabeki na kushikilia mpira unaweza kuwalazimisha mabeki wa Gaborone kucheza kwa tahadhari zaidi.
Kwa upande wa Gaborone, hilo linamaanisha kwamba hawatahitaji kumzuia Shalulile pekee, bali pia kuhakikisha kiungo na mabeki wanazuia huduma inayomfikia.
Mabadiliko ya vikosi
Gaborone United wameweza kubakiza sehemu kubwa ya kikosi kilichowapa mafanikio msimu uliopita, jambo ambalo linaweza kuwapa faida ya kuelewana. Hata hivyo, watamkosa beki Mothusi Johnson kutokana na majeraha, huku Benson Mangolo akitarajiwa kuchukua nafasi yake.
Hilo linaweza kuwa eneo ambalo Yanga watajaribu kulilenga, hasa kama wataweza kutumia kasi ya wachezaji wao wa pembeni kumvuta Mangolo kutoka kwenye nafasi yake.
Yanga nao wanaingia na silaha kubwa katika safu ya ushambuliaji kupitia Shalulile na Stephane Aziz Ki ambao uzoefu mkubwa katika mashindano ya CAF.
Nini Kinaweza Kuamua Mchezo?
1. Kasi ya mchezo:
Yanga wanaweza kutaka mchezo uwe na kasi, wakati Gaborone wanaweza kupendelea mchezo wa tahadhari na kuvizia nafasi.
2. Mipira ya kutenga:
Kwa kuwa Gaborone wanaaminika kuwa tishio kwenye set-pieces, Yanga wanahitaji kuwa makini katika kona na free-kicks.
3. Counter-attacks:
Gaborone wakifanikiwa kuiba mpira katika maeneo ya juu, Yanga wanaweza kuadhibiwa. Hivyo, rest-defence ya Yanga itakuwa muhimu.
4. Bao la kwanza:
Ikiwa Yanga watafunga mapema, Gaborone watalazimika kutoka zaidi na hilo linaweza kuwapa wageni nafasi zaidi. Lakini Gaborone wakifunga kwanza, mchezo unaweza kubadilika na kuwa mgumu zaidi kwa Yanga.
Hata hivyo licha ya Yanga kuwa ugenini, bado inapewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo hasa kama kocha Manqoba Mngqithi ataingia kwenye mchezo huo akiwa na mbinu sahihi. Tathmini ya vikosi inaonyesha Yanga ina kikosi bora zaidi kuliko wapinzani wao lakini pia Wananchi wana uzoefu mkubwa zaidi kwenye mashindano ya CAF kuliko wapinzani wao.